TRA YAKAMATA MIFUKO 40 YA SUKARI NA VIGAE


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Idara ya Forodha, imekamata mali ya magendo iliyokuwa ikiingizwa nchini kinyemela kupitia bandari bubu ya Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Naibu Kamishna wa Forodha, Patrick Kisaka ametaja mali hizo kuwa ni mifuko 40 ya sukari kutoka Brazil, ndoo 20 za mafuta ya kupikia kutoka Mashariki ya Mbali na katoni 70 za vigae, ambavyo maofisa wa TRA kwa kushirikiana na askari wa doria, walivikamata Januari 8 katika  bandari hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna huyo aliwataka wananchi hususan wanaoishi maeneo ya mipaka na ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kutojihusisha na biashara ya magendo na badala yake kuwafichua watu wanaofanya biashara hizo ambao wanaikosesha Serikali mapato.
“Tunaomba watu wanaojihusisha na biashara hizi waache mara moja kabla hawajaangukia mikononi mwetu kwani tutawachukulia hatua za kisheria zikiambatana na kifungo au faini, na huu ni kwa mujibu wa sheria.” Alisema Kamishna huyo.
Aidha, Kamishna huyo aliwataka wananchi watoe taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia namba 0789 933 8930 na 0789 338 931 endapo watabaini kuna vitendo vyovyote vya kimagendo hasa kwenye maeneo ya mipaka, ambako biashara hiyo imekuwa ikifanyika kwa kasi na kuahidi zawadi nono itakayolingana na kiwango cha kodi ya bidhaa hiyo.
Kisaka aliwahakikishia wananchi kuwa  idara yake kwa kushirikiana na askari wa doria wataendelea kupambana na wafanyabiashara wa magendo katika maeneo ya majini na nchi kavu usiku na mchana ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yake, ambayo yamekuwa yakipotea kwa njia hizo za kimagendo.
‘Sisi tutaendelea kupambana na magendo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutumia rasilimali zetu za nchi kavu na majini. Wenzetu wana boti sisi tutaweka mafuta na kufanya doria katika mipaka yote ya majini na nchi kavu”, alisisitiza Kamishna huyo.
Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, TRA kupitia idara hiyo imeshakamata mifuko 1158 ya sukari ya kilo 50 kutoka nje ya nchi, iliyokuwa ikiingizwa kwa magendo nchini kupitia doria zake mbalimbali zilizoko maeneo ya mipakani na kuahidi kuendeleza mapambano hayo.
Bandari bubu zinazotajwa kuwa ni kinara wa kupitisha bidhaa kimagendo ni Kunduchi na Ununio jijini Dar es Salaam na Mlingotini ya Bagamoyo.

No comments: