RC ATOA SIKU 5 ALBINO ALIYEPORWA APATIKANE AKIWA HAI


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ametoa siku tano kuanzia juzi Jumatatu kwa watendaji, sungusungu na wakazi wa kijiji cha Ndami, tarafa ya Mwambashimba wilayani Kwimba kuhakikisha mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel (4) aliyeporwa na watu wasiojulikana anapatikana akiwa hai ama mwili wake.

Alitoa agizo hilo  wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho na watendaji wa wilaya ya Kwimba ambapo alisema mazingira hayaoneshi kama mlango ulipigwa jiwe kubwa maarufu kama ‘fatuma’.
Alisema Kwimba ina watu 74 wenye ulemavu wa ngozi huku mtoto Pendo jina lake likiwa la tisa, lakini inashangaza kusikia siku ya tukio, Desemba 27 mwaka jana majira ya saa 3 usiku sungusungu wote walikwenda kula na muda mfupi baadaye mtoto huyo aliibwa baada ya kuvamia nyumba aliyokuwamo.
Alihoji maelezo ya sungusungu hao kwamba siku hiyo, wakati wa mchana walionekana watu wanne wasiofahamika wakiwa na pikipiki, lakini hakuna aliyechukua tahadhari ilhali wakijua kijijini hapo kuna mtu mwenye ulemavu wa ngozi.
“Hii hainiingia akilini, mimi nasema hapana kwa sungusungu na wanakijiji wote, lipo jambo halijafanyika na kwa imani yangu Pendo yupo salama na apatikane ndani ya siku tano, Ijumaa nitarudi hapa,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mulongo alitaka kila mmoja ajiulize katika nafsi yake, Pendo yupo na kwanini watu wengine wapo salama na bado watendaji wote wanaongea lugha inayofanana.
“Jambo la hovyo ni mazingira tuliyosoma kwenye eneo la tukio kuwa wahusika walikwenda na ‘fatuma’, lakini hakuna mazingira yoyote yanayoonesha kuwa fatuma lilitumika, hakuna nguvu iliyotumika bali yapo mazingira mnayafahamu, hata viongozi wa eneo hilo wanataka kutuaminisha hivyo,” alisema na kuongeza:
“Leo tarehe 5 (juzi), nasema hakuna kulala natoa siku tano kuanzia leo hadi Ijumaa Pendo apatikane, sungusungu maneno yasiwe mlikwenda kula chakula, mnatokaje kwenye lindo wote kwa pamoja, nataka kumuona Pendo akiwa mzima, najua.
Aliongeza: “Hamuwezi kujitangaza wenyewe kuwa ni watu wakatili, mazingira yanaonesha tukio limetengenezwa na hatuwezi kuwa na kijiji kisichoona uchungu kwa binadamu mwenzao, mhusika mnamjua na mnamficha”.
Alisema dunia nzima inawatazama watu wa Kwimba na Mwanza kwa ujumla kama watu wa hovyo wasio na utu hata kidogo kutokana na uzembe wa watu wachache, huku akisisitiza hatakubali mambo hayo yaendelee kutokea.
Alisema jambo hilo halihitaji itikadi ya vyama vya siasa, bali kuona maisha ya Pendo yanaokolewa.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema haiwezekani mtu kutoka mbali kufika katika eneo hilo na kumchukua mtoto Pendo bila kuongozwa na mwenyeji, hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.
Alisema Serikali ina mkono mrefu hivyo waliofanya kitendo hicho lazima watapatikane na kwamba Jeshi la Polisi halitolala hadi mtoto huyo apatikane akiwa hai au mwili wake.
Mtoto Pendo aliporwa na watu wasiojulikana usiku wa Desemba 27 majira ya saa 4.30 usiku katika kijiji Ndama wilayani Misungwi baada ya watu hao kuvunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa maarufu kama ‘fatuma’.
Watu 15 akiwamo baba mzazi wa mtoto huyo wanashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa uchunguzi zaidi.

No comments: