MTAMBO WA MAJI RUVU JUU KUZIMWA KWA SIKU MBILI


Shirika la Maji Safi  na Maji Taka jijini Dar es Salaam (Dawasco) limezima mtambo wa Ruvu Juu kwa siku mbili, kutokana na kuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu, ikihitaji  kubadilishwa, jambo litakalosababisha baadhi  ya maeneo kukosa huduma ya maji.

Ofisa Uhusiano wa  Shirika  hilo, Eva Lialo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia ubadilishaji wa vifaa hivyo katika mtambo huo  na kuongeza kuwa  marekebisho yalianza kufanyika tangu jana na leo.
Alisema  matengenezo hayo yamekuwa ya haraka na dharura huku wakibadilisha vifaa vingine, ambavyo vilikuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu.
Alisema pia katika marekebisho hayo, watabadilisha nguzo zinazoshikilia mita ambazo zimelala sana na kuhatarisha usalama katika eneo husika.
"Kutokana na hali hiyo Shirika litafanya matengenezo hayo kwa haraka kwa siku mbili ambayo italazimu kuzima kabisa mtambo huo  kwa siku mbili kwa masaa saba hadi 10,” alisema Eva.
Alisema kutokana na matengenezo hayo maeneo yafuatayo yatakosa maji kwa wakati huo ambayo  ni maeneo ya  Kimara, Mbezi, Makuburi, External, Mlandizi, Mburahati, Msewe, Changanyikeni na hata Kibamba.

No comments: