MAJARIBIO GESI YA MTWARA KUFANYIKA MWEZI UJAO


Sasa ni rasmi kwamba, majaribio ya usafirishaji wa gesi asilia kutoka Mnazi-Bay mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, yanatarajiwa kuanza mwezi ujao.
Hiyo inatokana na kukamilika kwa kiasi kikubwa kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia.

Kutokana na hatua hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limeelezea kuridhishwa hatua hiyo, huku Mwenyekiti wake, Michael Mwanda akisema sasa ataanza kupata usingizi.
Kuthibitika kuanza kwa majaribio hayo mwezi ujao kumeelezwa na Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni tanzu ya TPDC, Kampuni ya Gesi ya Taifa (GASCO), Kapuulya Musomba wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya TPDC waliokagua maendeleo ya ujenzi huo mwishoni mwa wiki katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Walikagua vya kupokelea gesi Kinyerezi na Tegeta, Dar es Salaam, vituo vya udhibiti wa usalama wa miundombinu ya bomba vilivyojengwa kuanzia Mtwara hadi Dar es Salaam kwa umbali wa kilometa 30, kituo cha kupokea gesi cha Somanga Fungu wilayani Kilwa, MnaziBay mkoani Mtwara inakopatikana gesi na pia kijiji cha Madimba, Mtwara unakojengwa mtambo wa kuchakata gesi.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huko, Musomba alisema unakwenda vizuri na kwamba kwa hatua iliyofikiwa, sasa majaribio yanaweza kuanza mwezi ujao.
“Pamoja na changamoto kadhaa, naweza kusema tumefika pazuri na wakati wowote mwezi ujao majaribio ya kusafirisha gesi yanaweza kuanza…nia yetu ni kuhakikisha kama ilivyokuwa imepangwa, Juni mwaka huu tuwe tumekabidhi mradi kwa serikali,” alisema Musomba.
Kutokana na kauli hiyo ya msimamizi mkuu wa mradi, Mwanda alisema kutokana na kazi hiyo mradi huo utakamilika kama ulivyopangwa Juni, mwaka huu. Maelezo hayo yalimkuna Mwanda na kusema: “Tujaribu kuwaeleza wananchi juu ya maendeleo ya mradi, kwamba unakwenda vizuri. Binafsi nitaanza kupata usingizi maana shughuli ilikuwa ngumu na upinzani ulikuwa mkubwa. Sasa kazi inakamilika, tujitahidi kuwa wazalendo…”
Awali, Musomba alisema ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 506 umekamilika kwa asilimia 99 na wameshajaribu kwa kupitisha maji.
"Kwa upande wa ujenzi wa bomba umekamilika kwa asilimia kubwa, na wameshapitisha maji kuangalia kama kuna maeneo yanayovuja, kinachofanyika sasa ni kukausha maji hayo kazi ambayo itakamilika mwisho wa mwezi huu," alisema na kuongeza kuwa, miundombinu mingine kama majengo katika maeneo ya miradi na mitambo viko katika hatua za mwisho. Mradi huo unagharimu dola za Marekani bilioni 1.225, sawa na Sh trilioni 2.08 za Kitanzania .

No comments: