MAITI ZAIDI ZAOPOLEWA AJALI YA BOTI ZIWA TANGANYIKA

Jumla ya miili ya watu watatu waliozama ndani ya Ziwa Tanganyika baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kukumbwa na dhoruba na kuzama imepatikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Jafari Mohammed aliwaambia waandishi wa habari mjini Kigoma kuwa sambamba na kupatikana miili hiyo mitatu pia idadi ya waliookolewa imeongezeka.
Alisema kuwa kati ya miili hiyo mitatu mmoja ni wa mtu mwenye miaka inayokadiriwa kufikia 38 mwanaume na miili miwili ni ya watoto.
Kamanda Mohammed alisema idadi ya watu waliookolewa imefikia 73 kutoka 49 walioripotiwa awali.
Alisema kuwa kati ya watu waliookolewa miongoni mwao raia 58 wa Burundi, raia wanne wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Watanzania 11.
Hata hivyo alisema kuwa haijafahamika walipo watu wanne kama wamekufa maji au wamekimbia baada ya kuokolewa na kwamba uchunguzi kuhusu walipo watu hao unaendelea.
Sambamba na hilo, Kamanda Mohammed alisema kuwa polisi inawatafuta manahodha wa boti hiyo ambao wamekimbia baada ya ajali wakituhumiwa kubeba abiria katika boti hiyo iliyosajiliwa kubeba mizigo.
Aidha Kamanda huyo wa Polisi mkoa Kigoma alisema wanamtafuta mmiliki wa boti hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Akilimali mkazi wa Ujiji mjini Kigoma aweze kukabiliana na makosa ya kuendesha boti inayokiuka taratibu za SUMATRA.

No comments: