HAYA NDIYO ATAKAYOFANYA JANUARY MAKAMBA AKISHINDA URAIS


Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amebainisha sera zake pindi Watanzania watakapompatia nafasi ya kuiongoza Tanzania na kusisitiza kupambana na rushwa, urasimu, udini na ajira.

Aidha, Waziri huyo ambaye hivi karibuni alitangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama chake cha CCM, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, alitaja maeneo mengine atakayoyapa kipaumbele katika uongozi wake huo.
Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na nishati miundombinu, mikopo, kanda ya kiuchumi, afya, huduma za maji, elimu, matatizo ya walimu na maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Katika mahojiano aliyoyafanya na Padri Privatus Karugendo aliyeandika kitabu cha Mazungumzo ya January Makamba, alisema katika eneo la urasimu endapo atapatiwa fursa ya kuiongoza nchi hiyo atahakikisha anafumua upya mfumo wa utumishi na utendaji serikalini ili kukomesha urasimu uliokithiri serikalini.
“Katika kufanya hili, ni lazima tuongozwe na misingi ifuatayo: Kwanza, uwajibikaji. Kwa sasa, ni vigumu sana kuwawajibisha watumishi wa umma kwa uzembe, ubadhirifu au kutotimiza wajibu wao. Tubadilishe Sheria ya Utumishi wa Umma ili kupunguza mlolongo wa kufikia maamuzi ya kuwawajibisha watu,” alisema January.
Katika eneo la rushwa, alisema kutokana na hali ya sasa ya rushwa kukithiri nchini, endapo atapatiwa nafasi anatarajia kufumua na kujenga upya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mifumo na sheria za kudhibiti na kuadhibu vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.
Alisema katika mabadiliko hayo makosa ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma yatakuwa ni makosa ya uhujumu uchumi na uhujumu wa taifa, na adhabu yake itaongezeka.
Kuhusu ajira January alisema eneo hilo linahitaji msukumo na hatua za kimapinduzi, na sio maneno tu ya kurudia kauli kwamba ajira kwa vijana ni bomu, lakini  bila kutoa ufumbuzi.
Alipendekeza hatua za kumaliza tatizo hilo kuwa ni Bunge lipitishe Muswada Maalum, Muswada wa Matumizi kwa Uwezeshaji Kiuchumi kwa Vijana, ambao utakuwa ni sheria maalumu ya matumizi ya Sh trilioni 3.6 kwa ajili ya mkakati wa miaka mitatu wa kupanua ajira kwa kuchochea shughuli za uzalishaji mali na uchumi.
“Katika eneo la elimu, kwanza nitahakikisha mjadala uliopo kuhusu dira ya elimu, ni elimu gani, ya aina gani na katika lugha ipi – tunataka watoto wetu wapate? Ni nini maana na malengo ya elimu nchini mwetu? Tukimaliza mjadala huu na sote tukakubaliana kama taifa, tutaondokana na changamoto ya kubadilisha mtaala mara kwa mara kama ilivyo desturi sasa,” alisema.
Aidha alisema iko haja ya kuanzisha Wizara mahususi ya Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam ili kuwezesha miradi mikubwa ya uwekezaji katika jiji kutekelezwa kwa haraka.

No comments: