BOTI YAKATISHA SAFARI PEMBA KUHOFIA MAWIMBI MAKALI BAHARI YA HINDI

Boti ya Royal Express I imelazimika kukatisha safari yake kisiwani Pemba kufuatia hali mbaya ya hewa iliyochafua bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makali baharini humo.

Boti hiyo iliondoka katika gati ya Malindi Saa 1:00 asubuhi leo lakini ilipofika maeneo ya kisiwa cha Tumbatu majira ya Saa 2:40 ikakatisha safari kutokana na kuchafuka kwa bahari.
Meneja Operesheni, Kapteni Sultan Alawi alithibitisha kukatishwa kwa safari ya boti hiyo alipozungumza na mwandishi katika bandari ya Malindi mjini Unguja.
Alisema kutokana na kuendelea kuchafuka kwa bahari wakati wakiendelea na safari ambapo mawimbi na upepo mkali uliokuwa ukivuma kwa kasi kubwa hakuwa na jinsi ila kulazimika kuirejesha boti hiyo ili kuokoa maisha ya abiria na mali zao.
Aliongeza kwa kusema kutokana na hali hiyo boti hiyo ilifanikiwa kufika katika bandari ya Malindi majira ya Saa 3:45 asubuhi kwa ajili ya kushusha abiria hao wapatao 345 wakiwamo watoto 61.

No comments: