BEI ZA PETROLI, DIZELI, MAFUTA YA TAA ZASHUKA


Bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, imeshuka kuanzia kesho, huku watumiaji wa petroli wakipata nafuu zaidi kutokana na kuuzwa chini ya Sh 2,000 baada ya kipindi cha muda mrefu.

Kutokana na kushuka kwa bei ambako pia kunachangiwa na kushuka kwa bei katika soko la dunia, sasa petroli itauzwa lita moja kwa Sh 1,955, dizeli itakuwa Sh 1,846 kwa kila lita moja na mafuta ya taa yatakuwa yanauzwa kwa Sh 1,833 kwa kila lita moja.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi alipokuwa akizungumzia mwenendo wa bei za mafuta nchini pamoja na utangazaji wa bei mpya za mafuta.
Alisema kuanzia kesho kutakuwa na punguzo la Sh 74 kwa petroli, Sh 62 kwa dizeli na Sh 54 kwa mafuta ya taa.
“Kwa bei ya kesho (leo) katika soko la Dar es Salaam hakutakuwa na mafuta ya zaidi ya Sh 2000. Kutakuwa na punguzo la Sh 74 kwa petroli, Sh 62 kwa dizeli na Sh 54 kwa mafuta ya taa,” alisema.
Alisema gharama za mafuta yatakayokwenda mikoani zitaongezeka kutokana na usafiri.
Alisisitiza kuwa, Ewura itahakikisha kuwa gharama zilizotangazwa ndizo zitakazotumika kwa wananchi.
Mkurugenzi huyo alisema bei ya mafuta ya mwezi Januari nchini, ni bei katika soko la dunia iliyotumika mwezi mmoja uliopita.
“Kwa Tanzania bei ya Desemba ni ya mafuta ya Oktoba hapa nchini na bei za Novemba ndizo zitatumika kesho (leo) hapa nchini,” alisema.
Alisema katika kipindi cha robo ya mwisho wa mwaka kuanzia Septemba hadi Desemba mwaka jana, bei za mafuta ghafi zimekuwa zikishuka kwa kasi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, bei zimeshuka kutoka dola 100 (Sh 170,000) kwa pipa hadi kufikia wastani wa dola 60 (Sh 102,000) kwa pipa moja ambayo ni sawa na kushuka kwa bei kwa  asilimia 40.
Kwa maelezo yake, asilimia ya kushuka kwa bei katika soko la ndani ni tofauti na kushuka katika soko la dunia kwa sababu mchango wa bei za soko la dunia katika bei za soko la ndani ni takribani asilimia 60.
“Gharama nyingine kodi za serikali, gharama za usafirishaji, gharama za usambazaji na gharama za upokeaji mafuta ambazo huchangia katika bei hazikushuka kwa sababu hazitegemei kushuka kwa bei za soko la dunia,” alisema.

No comments: