ANAYETUHUMIWA KULIPUA BASI LA KILIMANJARO EXPRESS KUKABIDHIWA TANGA

Mkazi wa mtaa wa Kitianjala mkoani Arusha, Efatar Molel (45) anatarajiwa kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga leo(kesho) kwa tuhuma za kusafirisha milipuko isivyo halali.

Milipuko hiyo 475 (baruti) ilikuwa kwenye maboksi matatu makubwa ikisafirishwa kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam ndani ya buti la basi namba T. 491 ARB la Kampuni ya Kilimanjaro Express.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alisema Januari 11 mwaka huu askari wa doria wa barabara kuu ya Mombo-Segera katika kijiji cha Chekelei cha wilayani Korogwe walikamata mzigo huo.
Aidha alisema kwa kuwa mhusika hakuwepo eneo la tukio ilibidi kutumia mawasiliano ya kiintelijensia kupata taarifa zake ambapo muda mfupi baadae ilibainika kwamba mmiliki wa mzigo huo ni Efatar Mollel anayeishi Kitianjala jijini Arusha.
“Milipuko hii inafanana na ile inayotumika kwenye shughuli za ulipuaji wa miamba na migodi ya madini, lakini tumebaini hii haina chaja (kichocheo) zake za kuwashia ingawa kwa namna ilivyo hapa ikikutana na moto inaweza kulipuka tu kwa urahisi”, alisema.
Alibainisha, “Nasema kwamba milipuko hii imesafirishwa isivyo halali kwa sababu haikuambatana na nyaraka za aina yoyote zinazoweza kuhalalisha mzigo huo… naamini tutakapompata mhusika atatueleza mengi kama anayo leseni pamoja na matumizi hasa ikizingatiwa kwamba  Dar hakuna migodi ya uchimbaji madini”,  alisema Kamanda Ndaki.
Alisema tayari mtuhumiwa huyo amekamatwa na askari wa mkoani Arusha na sasa taratibu za kumleta Tanga zinaendelea ili aweze kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Katika tukio jingine linahusisha kukamatwa kwa watu watatu wenye viroba 18 vya mirungi vyenye uzito sawa na kilo 440 ndani ya basi namba T. 244 BXQ la Kampuni ya Dar Express.
Kamanda Ndaki alisema wafanyabiashara watatu wa jijini Dar es Salaam wanatuhumiwa kuhusika na mirungi hiyo iliyokamatwa hapo Chekelei Januari 10 mwaka huu saa 8 mchana wakati basi hilo likisafiri kutoka mkoani Arusha kuelekea jijini Dar es Salaam.
“Wafanyabiashara wanaotuhumiwa ni Sara Mbwambo (38), Robinson Sam (24) ambaye ni kondakta wa basi hilo pamoja na Godfrey Machumbe (30) ambaye ni utingo wa basi… hawa wote ni wakazi wa Dar,” alisema.
Hata hivyo, Ndaki alisema watuhumiwa wamekiri mbele ya askari kwamba wanafanya biashara hiyo ya kusafirisha na kuuza mirungi, hivyo atapanda mahakamani wakati wowote kuanzia sasa baada ya upelelezi wa awali kukamilika.

No comments: