ABIRIA WAHOFIWA KUFA MAJI ZIWA TANGANYIKA

Watu saba wanahofiwa kufa maji na wengine 49 wameokolewa kutokana baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kukumbwa na dhoruba katika eneo la vijiji vya mwambao wa kusini wa ziwa Tanganyika.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Jafari Mohamed amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa boti ya mizigo ambayo ilikuwa imebeba watu zaidi ya 50 ilikuwa ikitokea mkoani Rukwa kuelekea nchini Burundi.
Hata hivyo taarifa ya Kamanda wa polisi mkoa Kigoma kuhusu vifo inapingana na taarifa iliyotolewa awali na watu waliozungumza na waandishi wa habari kutoka eneo la tukio .
Watu hao walisema watu saba wanahofiwa kufa wakati polisi ikieleza kuwepo na taarifa za kifo cha mtu mmoja.
Kamanda Jafari alisema kuwa boti hiyo ilikumbwa na dhoruba kati ya vijiji vya Sigunga na Herembe ambapo majira ya kati ya saa nane usiku na saa kumi alfajiri kuamkia jana.
Alisema kabla ya kukumbwa na dhoruba na kuzama abiria wakisaidiana na wafanyakazi wa boti hiyo walijaribu kutosa majini mizigo mbalimbali iliyokuwemo kwenye boti hiyo lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema upo uwezekano wa kuwepo kwa vifo
zaidi katika tukio hilo na tayari vikosi mbalimbali vya ukoaji vikihusisha polisi wanamaji, kikosi cha JWTZ cha wanamaji, SUMATRA na vikosi vya ulinzi na usalama vimeelekea eneo la tukio.
Alibainisha kuwa juhudi za boti za wavuvi waliokuwa kwenye shughuli zao za uvuvi zilisaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na hali ya uokoaji na kuweza kufanikisha kuokolewa kwa watu hao 49.
Kwa wiki nzima alisema  kumekuwa na hali ya hewa mbaya kwenye mwambao wa kusini wa ziwa Tanganyika unaoambatana na mawimbi na dhoruba kali.

No comments: