WATU 21 WANUSURIKA KIFO AJALINI WAKITOKA HARUSINI


Mtu mmoja amekufa na wengine 21 kujeruhiwa, baada ya basi dogo aina ya Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Shinyanga kwenye harusi, kurejea nyumbani kwao Morogoro kupinduka katika kijiji cha Ikugha wilayani Ikungi kwenye barabara kuu ya Singida - Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi (pichani) akizungumza kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, walikolazwa majeruhi, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Jumamosi iliyopita majira ya saa 8.00 mchana.
Alisema kuwa ajali ilitokea baada ya Coaster hiyo, kuhamia upande wa kulia wa barabara, kukwepa uharibifu uliotokana na kungoka mkanda wa chuma kwenye eneo hilo la daraja, hivyo kusababisha kugongwa kwa nyuma na  basi la Zuberi lililokuwa likipita kwa kasi.
Jina la dereva wa basi hilo la Zuberi, lenye namba za usajili T 983 ABU, lililosababisha Coaster hiyo kupoteza mwelekeo na kupinduka mara tatu, halijafahamika.
Jina la aliyekufa kwenye ajali na majeruhi, hayakuweza kupatikana mara moja.
Ajali hiyo imetokea kipindi ambacho kikosi cha usalama barabarani, kimeimarisha doria sehemu mbalimbali nchini.
Walioshuhudia ajali hiyo, walisema kuwa mwendo kasi na  uzembe wa madereva, bado ni kikwazo kwa usalama barabarani.

No comments: