WANANDOA WAUAWA KWA KUCHARANGWA MAPANGA MKOANI MARA...

Watu wawili ambao ni wanandoa wameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana na kisha wauaji hao kuchukua baadhi ya viungo vyao katika kitongoji cha Mwabasabi, wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi alithibisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia Desemba 24 mwaka huu.
Kamanda Kalangi aliwataja waliouawa kuwa ni Maduhu Mizingo ambaye ni mlemavu wa macho na mkewe aliyekuwa anamuongoza, Zawadi Sarehe (56), wote ni wakazi wa kijiji cha Mcharo wilayani hapa.
Imeelezwa, watu hao waliuawa na watu hao wakati wakitoka kusaga nafaka katika kijiji hicho majira ya saa 2:00 usiku.
Taarifa za awali kutoka katika kijiji hicho zinasema mauaji hayo yanatokana na mgogoro wa ardhi, ambapo kesi ya mgogoro huo iko mahakamani na watu wanaodaiwa kufanya mauaji hayo wake zao wanashikiliwa na polisi baada ya waume zao kukimbia.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Matwiga Muga, aliwataja watu wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo ya kinyama kuwa ni mwalimu mstaafu Charles Mgogo na kijana wake Lunyangi Charles ambapo wote ni wakazi wa kijiji hicho na kwamba wametoroka.
Alisema waliouawa walikuwa na mgogoro wa ardhi yenye ukubwa wa ekari moja na watuhumiwa hao, kwa kipindi kirefu, ikiwa ni pamoja na kumshambulia kwa kipigo mara kwa mara mlemavu huyo wa macho na kesi kufikishwa kwenye ofisi yake na kisha mahakamani.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Waziri Kingi na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Betysheba Maingu, walisema mauaji ya wanandoa hao yaligunduliwa na mtoto wao wa kiume aliyekuwa anakwenda shambani majira ya asubuhi.
Ilielezwa kuwa, mtoto huyo baada ya kufika katika eneo hilo aliuona mwili wa baba yake ukiwa umetelekezwa pembezoni mwa barabara, huku marehemu akiwa ameshikilia fimbo aliyokuwa anaitumia kumwongoza.
Aidha, ilielezwa kuwa kijana huyo alipokagua katika eneo hilo alibahatika kuuona mwili wa mama yake ukiwa umekunjwakunjwa baada ya kucharangwa mapanga na kufichwa pembezoni mwa kichaka jirani kabisa na nyumbani kwao.
Polisi walisema daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa mwanamke ulibainika kunyofolewa baadhi ya viungo vikiwemo sehemu zake za siri, macho, titi la kulia na makalio.
Aidha, alisema kuwa mwanamume huyo alikatwa panga kichwani na kutelekezwa katika eneo hilo ambapo mwili wake ulikutwa ukishambuliwa na wadudu wengi aina ya siafu.

No comments: