DEREVA WA BODABODA AUAWA NA KUTUNDIKWA KWENYE MTI


Mwendesha pikipiki (bodaboda), mkazi wa Kitongoji cha Buriba katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, Mrimi Nyabikwi (23), amekutwa amekufa na mwili wake kukutwa umening'inizwa kwenye mti maeneo ya Makaburini.
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa amethibitisha kifo hicho. Alisema habari kutoka ndani ya familia ya  mtu huyo zilidai kuwa Mrimi alitoweka nyumbani kwake kuanzia Desemba 24, mwaka huu.
Alisema marehemu alikuwa amekodisha pikipiki ya mkazi wa Sirari kwa kufanyia kazi ya kusomba abiria, lakini hakurejea nyumbani hadi mwili wake ulipokutwa na wachungaji wa mifugo maeneo ya makaburi katika mji huo wa Sirari. Mwili wa mtu huyo ulikuwa umeanza kuharibika.
Alisema kuwa mwili wa mtu huyo, ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya na kisha kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa maziko.

No comments: