Hisa
za benki ya biashara ya Mkombozi, jana
ziliingia kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kishindo huku bei yake ikipanda kwa
asilimia 50 kutoka Sh 1,000 hadi 1,500.
"Haya ni
mafanikio makubwa kwa benki yetu...kama nilivyosema mwanzoni wanahisa na
watanzania kwa ujumla wana imani na matarajio makubwa kwenye hii benki,"
alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mkombozi, Masha Mshomba.
Mshomba alisema
benki ya Mkombozi japokuwa ina muda mfupi tangu kuanzishwa kwake, imeonesha
mafanikio makubwa na huku ikikua kwa kasi kubwa.
Alisema benki hiyo
ilitegemea kupata Sh bilioni 5 kutokana na mauzo ya hisa 5,000,000, lakini
ilifanikiwa kuuza hisa 3,780,000 na kupata Sh bilioni 3.78 kwa kipindi cha wiki
tatu za mauzo ya hisa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa DSE, Moremi Marwa,
akiikaribisha Benki ya Mkombozi sokoni, alisema soko limejipatia mafanikio
makubwa mwaka huu kuliko wakati wowote tangu kuanzishwa kwake miaka 16
iliyopita.
Benki ya Mkombozi
inakuwa kampuni ya 21 kuuza hisa katika soko la Dar es Saalam na kuupandisha
mtaji wa jumla wa soko kwa makampuni yote na kufikia Sh trilioni 21.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport, Gaudence Temu alisifia
uamuzi sahihi wa benki ya Mkombozi kuingia kwenye soko la hisa, ambapo alisema
kuna faida nyingi za kibiashara.
"Tofauti na
urahisi wa kupata mtaji kwa ajili ya biashara, kwenye soko la hisa kuna unafuu
wa kodi lakini pia kuna umaarufu. Siyo kila kampuni inaweza kuuza hisa kwenye
soko hili na hivyo basi uwepo wenu humu ni kielelezo kuwa benki yenu inakidhi
vigezo," alisema Temu.
No comments:
Post a Comment