AJALI YAUA WANNE MOSHI, YAJERUHI WATATU HANDENI

Watu wanne wamekufa na watatu wamejeruhiwa katika ajali mbili tofauti, zilizotokea Moshi mkoani Kilimanjaro na Handeni mkoani Tanga.
Katika ajali ya Moshi, watu wanne wamefariki papo hapo na wengine watano kujeruhiwa  baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Moshi kwenda Same, kupata ajali eneo la Uchira, Moshi Vijijini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 30, mwaka huu saa 7 mchana katika eneo la Uchira na ilihusisha basi la Kilenga, lililokuwa likielekea Same.
Kamwela alisema basi hilo liligongana na gari dogo aina ya Toyota Hiace, lililokuwa likitokea Mwanga kwenda Moshi.
Alisema taarifa kamili kuhusu ajali hiyo, ambayo chanzo chake ni kupasuka kwa gurudumu la basi la Kilenga, itatolewa baadaye kwani bado hajapata namba za magari hayo na idadi kamili ya watu waliojeruhiwa.
Kwa ajali ya Handeni, wakazi watatu wa mjini Handeni wamejeruhiwa vibaya kwa moto baada ya lori, T 870ASD, lililokuwa limebeba shehena ya mafuta ya petroli, kugonga nguzo na kulipuka.
Moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa wa mali, ikiwemo nyumba tano za makazi, vibanda 16 vya biashara, pikipiki moja, magari matatu na banda lenye kuku 31.
Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo, Mariamu Mussa, alisema muda mfupi baadaye kasi ya moto unaowaka iliongezeka, kutokana na mafuta yaliyokuwa yakichuruzika kwenye mtaro wa jirani na lori kuelekea kwenye nyumba. 
“Mafuta hayo yalisababisha mlipuko mkubwa wa moto ambao ulienea
kwa urahisi mpaka kufika kwenye nyumba na vibanda vya maduka yanayouza nguo na bidhaa mbalimbali huku tukishindwa kuuzima kwa kuhofia usalama wa uhai wetu”, alisema.
Shuhuda mwingine aitwaye Mrisho Makata alisema moto huo, ulisababisha taharuki kwa wakazi wa Chanika na wa maeneo ya jirani, wakiwemo  wale  waliounguliwa nyumba zao na kusababisha hasira ipande, kiasi cha kuthubutu kulipiga kwa mawe gari la Zimamoto na Uokoaji, lililoazimwa na uongozi kutoka wilayani Korogwe, wakidai kwamba limechelewa kufika eneo la tukio. 
“Chanzo cha ajali inaonekana gari hilo la mafuta, linaonekana lililemewa sana na mzigo kiasi hata likamshinda dereva…lilionekana katika  baadhi ya maeneo kama linayumbayumba sana wakati lilipokuwa likitaka kukata kona…lakini pia inawezekana lilikuwa na hitilafu za kiufundi, kwa sababu liliyumba sana kabla ya kugonga nguzo na tatizo ni kwamba haya magari makubwa wakati mwingine hata matengenezo hayafanyiwi, inatisha sana”, alisema shuhuda huyo. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea majira ya saa 3.25 jana asubuhi katika eneo la Kivesa kata ya Chanika mjini Handeni katika barabara kuu ya Handeni kuelekea wilayani Kilindi. 
“Chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo ‘tanker’ lililokuwa limebeba mafuta wakati linafika eneo la tukio, lilikutana na pikipiki ya bodaboda ambapo dereva alipotaka kuikwepa, aligonga nyumba moja pamoja na nguzo ya umeme iliyokuwepo jirani”, alisema. 
Alitaja waliojeruhiwa ni Mohamed Athumani (20), mkazi wa Kivesa, ambaye alikuwa Utingo wa lori hilo na kwamba ameungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha alazwe katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Bombo iliyoko jijini Tanga.
Wakazi wengine wa mjini Handeni waliojeruhiwa kwa moto kwenye ajali hiyo ni Ali Said (50), mkazi wa Chogo na Zuberi Salehe (24) ambaye ni mtumishi wa Kituo cha Mafuta kinachomilikiwa na mfanyabishara mwenye lori hilo, lililopata ajali. 
Akizungumzia uharibifu huo, Kashai alisema moto umeteketeza ‘cabin’ya lori la mafuta, gari namba T 915 BDE Toyota Canter, mali ya John Shayo na pikipiki aina ya Watco yenye namba T724 BEE. 
“Madhara yaliyotokana na ajali hiyo kwa kweli ni makubwa sana hasa ikizingatiwa kwamba kuna gari la Zimamoto aina ya Isuzu, ambalo ni mali ya halmashauri ya wilaya ya Korogwe limeharibiwa vibaya na wananchi waliokuwa eneola tukio kwa kutumia mawe, mara tu lilipowasili hapo kwa lengo la kutoa msaada”, alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo, Mkuu wa Wilaya, Muhingo Rweyemamu alisema tukio hilo limemsikitisha sana. Pia, alisema amesikitishwa na kitendo cha wananchi hao kuamua kuliharibu kwa mawe gari hilo la halmashauri ya Korogwe. 
“Kwa kweli ni kitendo cha aibu na ajabu sana kilichofanywa nawananchi
Hawa, hasa ikizingatiwa kwamba wote wanafahamu kwamba wilaya ya Handeni haina kabisa gari la Zimamoto wala vifaa vya kuzimia moto. 
“Uongozi umefanya jitihada za kuazima gari Korogwe, lakini wao hawakuona hilo, badala yake wameliharibu kwa mawe, eti kwa sababu limechelewa kufika. Hivi kweli kwa akili za kawaida gari lingewezaje kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 70 na mzigo wa maji kwa mwendo kasi wa kufika haraka eneo la tukio? Hili halikubaliki.”, alisema. 
Aidha, alisema ajali hiyo imetoa fundisho kubwa kwa viongozi na wananchi wilayani humo, kwamba ni shida kwa mji mkubwa kama Handeni,  kukosa gari la zima moto na kusema jitihada za haraka zitafanywa ili kumaliza tatizo hilo.
Muhingo alisema tathmini ya kubaini gharama halisi ya uharibifu huo, bado haijafanyika na kwamba tayari watu kadhaa wanahojiwa ili kuwabaini waliosababisha uharibifu wa gari hilo. 

No comments: