WAWEKEZAJI WA GESI NA MAFUTA WAMIMINIKA ZANZIBARSerikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema taasisi mbalimbali za kimataifa zinazojishughulisha na masuala ya mafuta na gesi zimeanza kujitokeza kuomba fursa ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Maombi hayo yamekuja kutokana na suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano katika mchakato uliomalizika hivi karibuni wa Katiba Inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Hayo yalisemwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipozungumza na wananchi wa jimbo la Kitope huko Kichungwani mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya kushiriki kazi za usambazaji majisafi na salama.
Balozi Iddi ambaye ni mbunge wa jimbo hilo alisema miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na wananchi wengi wa Zanzibar kuondolewa katika orodha ya Muungano ni suala la mafuta na gesi.
“Wananchi mambo ambayo tumeyapigania kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba yanaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano ni suala la mafuta na gesi,”  alisema.
Alisema hatua hiyo imeanza kuleta manufaa makubwa kutokana na baadhi ya wawekezaji, taasisi na mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na kazi za utafutaji wa nishati hiyo kuwasilisha maombi yao.
Aidha, balozi aliwataka wananchi kutokubali kuyumbishwa na kudanganywa na wanasiasa ambao hivi sasa wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuwababaisha wananchi na kupita kila sehemu wakidai kwamba katiba inayopendekezwa haina maslahi kwa wananchi wa Zanzibar.

No comments: