WAJASIRIAMALI 90 KUSHIRIKI MAONESHO LA BIASHARA MBEYA


Zaidi ya wajasiriamali 90 kutoka mikoa mbalimbali nchini wanatarajiwa kushiriki maonesho ya bidhaa za wajasiriamali ya Mbeya Trade Fair yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 19 kwenye viwanja vya Ruandanzovwe jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kampuni ya Mbeya Trade Fair(MTF) inayoandaa maonesho hayo, Newton Mwasabwite maonesho hayo yanayofanyika kwa mwaka wa tano sasa yanalenga kupanua wigo wa kibiashara kwa wajasiriamali.
Mwasabwite alisema pia kupitia maonesho hayo wajasiriamali wadogo wamekuwa wakipata fursa ya kukutanishwa na wafanyabiashara wakubwa na kupeana uzoefu na pia kuweka mikakati ya pamoja ya kimaendeleo kwa biashara zao.
Alimtaja mbunge wa viti maalumu mkoani Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa kuwa mgeni rasmi atakayefungua maonesho hayo Oktoba 14 na kwa siku zinazofuatia kila mkuu wa wilaya kwa wilaya za mkoani hapa atapata fursa ya kutembelea maonesho hayo kama mgeni rasmi wa siku husika.
Mwenyekiti huyo alisema ili kunogesha maonesho, sanaa za nyimbo na ngoma za asili za makabila mbalimbali zitakuwa zikioneshwa pia lengo likiwa ni kuzitangaza asili za kiafrika ambazo zinaonekana kusahaulika kadiri siku zinavyokwenda.

No comments: