POLISI YAZUNGUMZIA WIMBI LA UTEKAJI WATOTO DAR



Wakati hofu juu ya usalama wa watoto katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ikizidi kutanda miongoni mwa wazazi na walezi, Polisi imekanusha kuwapo kwa matukio ya utekaji nyara watoto wanaosoma shule za msingi na kufanyiwa unyama ukiwamo ulawiti, kuuawa na hata kuchunwa ngozi.
Kwa wiki kadhaa sasa, hofu juu ya matukio ya aina hiyo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za mitandao ya kijamii, ikielezea jinsi watoto wanavyotekwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza jana, alisema hivi karibuni umezuka uvumi kutoka kwa watu mbalimbali kwamba lipo kundi la wahalifu wanaotumia gari aina ya Toyota Noah yenye rangi nyeusi kutenda uhalifu dhidi ya watoto.
Alisema Polisi imefanya uchunguzi na mpaka sasa hawana taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa mtindo wa utekaji nyara. Kwa mujibu wa kamanda, polisi inamshikilia mtu mmoja kwa kuhusika kusambaza uvumi huo.
“Polisi imegundua kwamba huu ni uvumi ambao haujulikani chanzo chake hivyo nawaomba wananchi kuachana na uvumi huo na kupuuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi na kuleta usumbufu kwa baadhi ya watu,” alisema.
Alisema Oktoba 3 mwaka huu saa 3.00 asubuhi, Vingunguti, mfanyakazi wa The Guardian Ltd, Prosper Makame (34) akiwa na mkewe MaryStella Munis (30) mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika eneo la shule ya msingi Kombo kwa ajili ya kuchukua fedha  za vyombo wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba T 252 DAY rangi nyeusi na kuvamiwa na wananchi.
“Wakati watu hao wakisubiri kuchukua fedha, ghafla walikuja zaidi ya wananchi 100 na kuzingira gari hilo huku wakipiga kelele wakidai kwamba ndilo gari linaloteka wanafunzi. Lakini polisi walipata taarifa hizo mapema na kufika eneo la tukio na kuwaokoa watu hao pamoja na gari lao,” alisema.
Kova alisema Oktoba 13 saa 10.00 katika Kituo cha Polisi Tabata katika Manispaa ya Ilala, uliibuka uvumi kuwa gari namba T 548 BUN aina ya Noah nyeusi ambayo ni mali ya askari polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani, Inspekta Esther lililokuwa kituoni hapo, ndani yake kulikuwa na vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani.
“Kutokana na uvumi huo wananchi walikusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona hivyo vichwa vitano, ndipo mkuu wa kituo hicho alipoamuru gari hilo kufunguliwa na kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uongo na uvumi,” alisema.
Alisema hali hiyo ya uvumi ni ya hatari kwa sababu wananchi kila wanapoona Noah nyeusi wanaikimbilia na kuizingira kwa lengo la kufanya fujo.
“Polisi tunasisitiza kuwa uvumi huu wa kuwepo kwa kikundi cha wahalifu ambao wamekuwa wakiwateka watoto na wanafunzi siyo kweli hata kidogo na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema.
Alisema uchunguzi wa kubaini nani alieneza uvumi huo ulifanyika na kubaini kuwa umeenezwa na Gilbert Stanley (32), mkazi wa Tabata ambaye alikamatwa.
Alipohojiwa, kwa mujibu wa kamanda, alikiri kueneza habari hizo na kudai aliambiwa na mtu mwingine ambaye alidai hamkumbuki.

No comments: