PINDA KUZINDUA MRADI WA SAYANSI WA SHILINGI BILIONI 165


Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa wiki hii kuzindua mradi  wa sayansi na teknolojia wa elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temo alisema jana kuwa mradi huo unaogharimu  Dola za Marekani milioni 100 sawa na Sh bilioni 165 ulianzishwa mwaka 2008 na kuisha Julai 31 mwaka huu.
Alisema ziara ya Waziri Mkuu itaanza leo, akianzia Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoa wa Morogoro ambako atazindua miradi ya majengo mbalimbali yakiwamo ya kilimo na biashara, masomo ya chakula na teknolojia na uhandisi wa kilimo.
Kesho Waziri Pinda atatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM)  na kuzindua mradi wa majengo saba  mapya  na ukarabati  wa majengo matano  katika chuo hicho.
Alisema  kupitia mradi huo wameweza kuwasomesha walimu 120  kwa Stashahada  Uzamivu na Uzamili.
Kadhalika, Waziri Pinda atatembelea Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na kufungua majengo yaliyojengwa kupitia mradi huo. 
Profesa Temo aliongeza kuwa keshokutwa, Waziri Mkuu atatembelea  Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE)  ambapo atazindua jengo la kitaaluma la kuwaendeleza walimu na jengo jipya la maabara ya kemia.
Alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambao imeanzishawa tangu  kuanza kwa  uhuru hadi sasa.
 “Mradi huo umeweza kujenga majengo mapya 25, kurekebisha majengo, kusomesha walimu takriban 250, kuboresha maabara,  karakana na kuongeza vifaa vya mafunzo,” alisema Profesa Temo.
Chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia,  mradi umetajwa kuboresha  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), maktaba na pia kuboresha uongozi wa tasisisi mbalimbali za elimu na kuziunganisha katika mtandao  wa kitaifa.
Pia mradi huo umeboresha vyuo vikuu saba ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Morogoro, Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo Kikuu Ardhi na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce).

No comments: