Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imetenga Sh milioni 80 katika mwaka 2014/2015 kwa ajili ya kufanya utafiti kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa hospitalini hapo.
Hayo yamebainishwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela wakati wa ufunguzi
wa Baraza la Utafiti la hospitali hiyo, ambapo alisema, sambamba na kutengwa
kwa fedha hizo pia bodi iliridhia kuanzishwa kwa kitengo cha Mafunzo, Utafiti
na Ushauri.
"Leo ni kama
tunatimiza eneo la tatu la kuwa na tafiti nyingi, zenye ubora wa juu ambazo
zitasaidia katika kuboresha huduma tiba na kinga katika nchi yeti. Hivyo kama
hospitali kuu ya taifa tunategemea mwanzo huu mzuri leo utasaidia kufikia azma
hiyo," alisema Dk Njelekela.
Alisema hospitali hiyo
imekuwa ikitoa nafasi na ushirikiano kwa vyuo vikuu, mashirika na taasisi
mbalimbali kufanya tafiti zao katika hospitali hiyo.
Alisema katika majukumu
aliyoagizwa moja ni kuhakikisha madaktari na wafanyakazi kutoka maeneo mengine
wanaongeza morali ya kufanya tafiti na kuongeza idadi ya tafiti hospitalini
hapo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Baraza la Utafiti na Taifa, Dk Rose Kingamkono ambaye alikuwa
mgeni rasmi alisema, baraza hilo litasaidia katika kufanya utafiti na hatimaye
kupata suluhisho la magonjwa mbalimbali, ikiwemo yale yasiyoambukizwa ambayo
kwa sasa yameongezeka kwa kasi.
Alisema magonjwa
yasiyoambukizwa yameongezeka kutokana na mtindo wa maisha wanayoishi watu wengi
jambo linalochangia magonjwa hayo. Alisema suala la chakula kwa kiasi kikubwa
limesababisha ongezeko la magonjwa hayo.
No comments:
Post a Comment