Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Septemba umepungua hadi
asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.7 ilivyokuwa Agosti mwaka huu.
Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi, Ephraimu Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko huo wa bei
kunamaanisha kasi ya upandaji wa bei za
bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Septemba imepungua ikilinganishwa na kasi
iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti mwaka huu.
Alisema pia kuwa fahirisi za bei
zimeongezeka hadi 149.93 mwezi Septemba mwaka huu kutoka 140.1 mwezi Septemba
mwaka jana.
Alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula
na vinywaji baridi umepungua hadi asilimia 8.5 mwezi Septemba mwaka huu kutoka
asilimia 8.8 ilivyokuwa mwezi Agosti mwaka huu.
Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko wa
bei wa mwezi Septemba mwaka huu, kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya
bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwezi Septemba.
Alisema bei za vyakula zilizoonesha
kupungua kwa mwezi Septemba ni pamoja na mchele, ulezi, mahindi, matunda na
sukari kwa asilimia 3.5. Alisema bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua
kwa bei mwezi Septemba 2014 ni sare za shule, simu za mkononi, runinga na
viatu.
Kwesigabo alisema mfumuko wa bei una
mwelekeo unaofanana na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Alisema Kenya mfumuko
umepungua hadi asilimia 6.6 mwezi Septemba kutoka asilimia 8.36 wakati Uganda
mfumuko umefikai asilimia 1.4 kutoka asilimia 2.8.
Kuhusu thamani ya shilingi, Kwesigabo
alisema uwezo wa Sh 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Sh
66 na senti 70 mwezi Septemba 2014 kutoka mwezi Septemba 2010.
No comments:
Post a Comment