Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameandaa maonesho na mdahalo wa kukumbuka na kuenzi mchango wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kujenga, kutetea, kulinda na kudumisha amani.
Maonesho hayo ya siku
tano ambayo yatafunguliwa Jumatatu na kumalizika Oktoba 17 yatafanyika katika
ukumbi wa Makumbusho ya Taifa yaliyopo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilisema maonesho hayo yatajikita zaidi
kuonesha picha, nyaraka, vitabu, matukio na kazi mbalimbali zinazohusu Baba wa
Taifa ambaye ni Rais wa Kwanza na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama ya Tanzania.
Mada zitakazotolewa
katika mdahalo utakaofanyika tarehe 17 ambayo
ndiyo siku ya kilele cha
makumbusho hayo ni misingi, utekelezaji na usimamizi wa kujenga, kulinda na
kudumisha amani na uchambuzi na mifano halisi ya Sera za utekelezaji wa misingi
ya kujenga amani kwenye Sekta mbalimbali za maendeleo.
“Lengo kuu la maonesho
na mdahalo huo ni kuwawezesha watanzania na hasa vijana kujifunza na kujua
misingi ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliizingatia katika kujenga,
kutetea, kulinda na kusimamia ili Tanzania iwe nchi ya amani kama ilivyo
leo na pia mchango wake alioutoa kudumisha amani”.
Baadhi ya misingi mikuu
aliyoizingatia ni utu, usawa, haki na heshima kwa binadamu wote. Misingi hii
iliifanya Tanzania iwe kitovu na mbeleko ya harakati za ukombozi wa Bara la
Afrika na utetezi wa haki za wanyonge duniani”, ilisema Taarifa hiyo.
Maonesho na mdahalo huo
vimeandaliwa ili viwe sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 tangu kifo cha Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilipotokea tarehe Oktoba 14, 1999
katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London nchini Uingereza.
Maadhimisho hayo kitaifa
yanafanyika mkoani Tabora.
No comments:
Post a Comment