Madaktari wataalamu
watano wa afya wamejitolea kwenda kutoa huduma katika baadhi ya nchi za Afrika
Magharibi zilizoathiriwa na ugonjwa wa ebola.
Wataalamu hao walioondoka jana, baadhi yao walizungumza na
waandishi wa habari katika mkutano kati ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan
Mmbando na vyombo vya habari.
Dk Mmbando (pichani) aliwataja kuwa ni Dk Justin Maeda kutoka Mvomero,
Dk Herilinda Temba kutoka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Shaban Sasita,
Godbless Lucas na mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko kutoka Lindi, Theophil
Malibiche.
Kwa mujibu wa Dk Mmbando, baada ya kuondoka jana, wamekwenda
Ethiopia ambako watapangiwa majukumu kwa
ajili ya kusaidia kukabili tatizo hilo.
Alisema wataalamu hao watafanya kazi kwa wiki tatu za awali
na serikali itaendelea kuwasaidia kutimiza majukumu yao.
Akizungumzia mchakato wa kupata wataalamu hao, alisema
walitangaza na baadae wakajitokeza hao ambao wamechaguliwa kwa ajili ya kwenda
kujumuika na wataalamu wengine kutoa huduma katika nchi hizo zilizoathiriwa na
ebola.
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa madaktari hao,
Dk Meeda alisema atakubali kukabiliana na hali yoyote katika kazi yake.
Alisema hiyo ni sehemu ya kupata uzoefu hatimaye atakaporudi
nchini, asaidie Watanzania endapo ugonjwa huo utajitokeza.
Daktari mwingine, Dk Temba alisema ana moyo wa kusaidia
wengine na ndiyo maana ameamua kujitolea kwenda kuhudumia waathirika wa ugonjwa
huo.
Awali, Dk Mmbando alisema ebola imekumba zaidi nchi za
Afrika Magharibi ambapo hadi sasa takwimu zinaonesha watu 7,500 wameugua ugonjwa huo.
“Watu 3,500 wamepoteza maisha kutokana na ebola. Ugonjwa huu
pamoja na kuwapata wananchi pia umegusa wataalamu wa afya na hauchagui,”
alisema Mganga Mkuu.
Aidha alisema, kwa upande wa hapa nchini, wanaendelea na
mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kama utajitokeza.
Alisisitiza ipo kamati ya kitaifa ambayo wanakutana kila wiki sanjari na
kutekeleza mpango katika ngazi mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu, wizara imetoa mafunzo jinsi ya
kuhudumia wagonjwa wa ebola. Hatua hiyo imekwenda sanjari na kutenga kituo
maaluma Temeke, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa ebola.
Katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege vimewekwa
vifaa maalumu kwa ajili ya kupima joto la mwili kama lipo juu. Alisisitiza
kinachopimwa siyo ebola kwa sababu ugonjwa huo unapimwa katika maabara
zilizopatiwa ithibati.
No comments:
Post a Comment