MABORESHO ELIMU YAONGEZA PhD MPYA 79 MLIMANI, CHUO KIKUU HURIAWakati Serikali ikipambana kuhakikisha wimbi la wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita nchini, wanapata fursa ya kujiunga na elimu ya juu, wanafunzi 9,649 wenye sifa ya kupata mikopo  ili wajiunge na elimu ya juu mwaka huu, wamekosa fursa hiyo.
Juzi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alielezwa kuwa Mradi wa Sayansi na Teknolojia ya Elimu ya Juu (STHEP) unaosimamiwa na Serikali, umesaidia kuongeza idadi ya wahadhiri wa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (Phd) 79 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na katika Chuo Kikuu Huria (OUT).
Kati ya wahadhiri hao 79, waliopata udhamini wa kusomea shahada ya uzamivu, wahadhiri 12 ni kutoka Chuo Kikuu Huria  na wahadhiri 67 ni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wakati Waziri Mkuu akipata taarifa hizo za maendeleo ya mradi huo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ilitoa taarifa jana ikieleza kuwa wanafunzi 9,649 wamekosa mikopo ingawa wana sifa.
Akizungumza kuhusu mradi huo baada ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji wake katika vyuo hivyo juzi, Pinda alisema lengo lake ni kujenga uwezo wa wataalamu kufundisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita, ambao kwa sasa ni wengi.
 “Mradi huu ni wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2009 na unakamilika mwaka huu. Lengo hasa ni kujenga uwezo wa wataalamu wetu ambao watakuja kufundisha watoto wa kidato cha sita ambao idadi yao inazidi kuongezeka kila mwaka,” alisema Pinda.
Alisema katika kukabiliana na tatizo la sasa la ongezeko la wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita, Serikali iliamua kukopa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB), ili kuboresha miundombinu kwenye taasisi za elimu ya juu nchini. 
Kwa mujibu wa Pinda, Serikali iliridhia pia fedha hizo zitumike kujenga miundombinu mipya ya kufundishia pamoja na kukarabati baadhi ya zamani kwani kama miundombinu haipo, kazi ya kufundisha haitakuwepo.
“Tulikubaliana pia fedha hizo zinunue vifaa kwa maana ya kompyuta, vifaa vya maabara pamoja na samani za maktaba na baadhi ya madarasa. Ni fedha za mkopo lakini zimetumika kusaidia Watanzania wote,” alisema.
Akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pinda alikagua majengo mapya ya ghorofa, ikiwemo jengo la Shule Kuu ya Elimu, Sayansi ya Majini ambalo litakuwa na kituo cha wanafunzi. Pia alizindua jengo jipya la Uhandisi Migodi na Usindikaji Madini katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia.
Akitoa taarifa ya miradi yote hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema katika awamu ya kwanza ya STHEP, chuo hicho kilipata Sh bilioni 67.
Profesa Mukandala alisema chuo kimefanikiwa kuendeleza kimasomo wafanyakazi wake zaidi ya 150, kujenga majengo mapya manane, kusomesha wahadhiri tarajiwa 163 ambapo 63 wamesoma shahada za uzamili  na 67 wamepata shahada za uzamivu (PhD).
“Tumenunua vifaa mbalimbali vikiwemo vya maabara, kompyuta 864, vitabu zaidi ya 960, na vifaa vya teknolojia, uhandisi na sayansi. Pia tumepanua madarasa, maabara na ofisi.
 “Tumepata maabara mpya 49 zitakazotumiwa na wanafunzi 3,630 kwa wakati mmoja; madarasa 53 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,200 kwa wakati mmoja; ofisi 322 zitakatumiwa na wafanyakazi wasiopungua 600,” aliongeza.
Akiwa katika Chuo Kikuu Huria, ambako alizindua jengo la ghorofa 10  lililopewa jina la Open Distance Learning Tower   (ODL Tower) lililogharimu Sh bilioni 3, Pinda alielezwa kuwa chuo hicho kimesomesha wahadhiri 29, kati ya 12 wamepata shahada za uzamivu na 17 shahada za uzamili.
Chuo hicho pia kimejenga maabara za kompyuta tatu, maktaba ya kuweka watu 224 kwa wakati mmoja, vyumba vya mihadhara  maabara ya lugha na kununua kompyuta na samani zingine.
Wakati vyuo vikuu vikifanya maboresho hayo kujiandaa kupokea wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu, taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha HESLB, imeeleza kuwa kati ya waombaji 42,227 waliojaza fomu za kuomba mkopo kwa usahihi, waombaji 39,793 walikuwa na sifa za kukopeshwa.
Hata hivyo kwa mwaka wa masomo 2014/2015, Bodi hiyo imeeleza kuwa uwezo wake ni kutoa mkopo kwa wanafunzi 30, 066 tu wa mwaka wa kwanza wanaosoma ndani ya nchi na wengine 78 wa mwaka wa kwanza wanaosoma nje ya nchi, na hivyo kuacha wanafunzi 9,649 wenye sifa bila mikopo.  
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waombaji wanaoendelea na masomo hawakutakiwa kujaza fomu za maombi ya mikopo hiyo. Aidha, orodha kamili ya waombaji wapya waliopangiwa mikopo ipo kwenye tovuti ya Bodi ambayo niwww.heslb.go.tz au www.olas.heslb.go.tz na muombaji anaweza kutafuta jina lake kwa kutumia namba ya mtihani ya kidato cha nne.

No comments: