MABASI YAGONGANA USO KWA USO NA KUUA ABIRIA WALIOKUWAMO



Watu wanne wamekufa na  wengine 14 wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda baada ya basi la Kampuni ya AN kugongana uso kwa uso na gari jingine.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo ilitokea jana nyakati za saa tisa  alasiri katika eneo la Mtamba wilaya ya Mlele mkoani humo katika barabara ya Mpanda - Tabora.
Aliwataja marehemu kuwa ni Emanuel Kavisha, mkazi wa kijiji cha Kasansa Tarafa ya Mamba wilaya ya Mlele  na mwingine alifahamika kwa jina moja la Mswaya, ambaye ni mkazi wa Tarafa ya Inyonga wilaya ya Mlele huku marehemu wengine wawili hawajafahamika majina yao.
Alisema ajali  hiyo ilihusisha  basi  aina  Scania   mali ya Kampuni ya AN  yenye namba za usajili T 502 ALG nililokuwa likitokea Tabora kuelekea Mpanda  na Costa yenye namba za usajili T 970 ASJ mali ya Emoro, mkazi wa Kerema Wilaya ya Mpanda, lililokuwa likiendeshwa na Abdu Feruzi likiwa linatokea Mpanda mjini  kwenda Tabora.
Aliwataja majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda kuwa ni Jafari Jackison, Leonald Patrick  (26) David Linus  (25), Donald Gabriel (43)  Nicolas Wilaamu  (25) wote wakazi wa tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele.
Wengine ni  Christopher Kapaya , Jackson Shila (15),  Joseph Chalula  (16) wakazi wa Wilaya ya Nkasi, Rukwa ambapo majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Kidavashari alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari hayo na dereva wa Costa alikimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo na jeshi la polisi linaendelea kumsaka.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Dk Jafari Kitambwa alisema hali ya majeruhi waliolazwa hospitalini hapo inaendelea vizuri.

No comments: