LUKUVI AMCHONGEA WAZIRI NYALANDU KWA KINANA


Mbunge wa Ismani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amemtaka Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kuhoji utendaji kazi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Ombi la Lukuvi kwa Kinana linatokana na kile alichosema ni kitendo cha waziri huyo kutojibu barua mbili alizoandikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma kuhusu  malalamiko ya wananchi dhidi ya mwekezaji wa kampuni ya utalii wa uwindaji ya Kilombero North Safaris.
“Wananchi walikuja kwangu mara mbili kule Dodoma kuhusu hili. Kuna barua mbili zimeandikwa kwa (Lazaro) Nyalandu na Mkuu wa Mkoa (Ishengoma) ambazo mimi nimetuma tena nakala zake mara tatu, lakini hakuna majibu yaliyotolewa,” alisema Lukuvi.
Aliendelea kusema; “Ukifika Dar es Salaam utuite pamoja na Nyalandu, nadhani wewe (Kinana) ukimwita utamfundisha kuwa viongozi wenzako wakikuandika, lazima ujibu.
“Najua huko atasema namshitaki lakini mimi ndio co-ordinator (mratibu) wa Serikali nasema yaliyo ya kweli,” alisema na kuongeza: “ Kama mkuu wa mkoa anaandika barua, halafu hajibu, haifai.”
Kwa mujibu wa Lukuvi, barua ya kwanza ni ya wananchi walioomba eneo la Lunda Mkwambi liondoshwe kama eneo la hifadhi na kuwa la ufugaji ambao wana uwezo wa kuchunga mifugo yao huku wakiwa walinzi wa wanyama.
Lukuvi alisema barua ya pili ni ya kumtaka Waziri Nyalandu kuingilia kati mgogoro kati ya Jumuiya ya Mbomipa na mwekezaji Kilombero North Safaris.
Alisema pamoja na viongozi wa Mbomipa, ‘kula bila kunawa’ katika kuingia mkataba huo, lakini waliokula zaidi ni watu wa wizara kwa sababu hakuna mkataba unaoingiwa bila wizara ya maliasili kufahamu.
“Wizara ya Maliasili na Utalii imehusika na kuwaingiza mkenge hawa watu wa Mbomipa,” alisema.
Awali, Mkazi wa Kijiji cha Idodi, Danny Salum alimwomba Katibu Mkuu Kinana kumwondoa mwekezaji Kilombero North Safari kwa kile alichodai ameshindwa kutekeleza ahadi zake za kutoa mapato, kujenga hoteli ya kisasa na kambi.
Alisema mwaka 2008, Mbomipa inayoundwa na vijiji 21 vya tarafa ya Pawaga na Idodi, vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, iliingia mkataba wa miaka 25 na mwekezaji huyo.
Alisema ikiwa ni zaidi ya miaka mitano imepita tangu mwekezaji huyo aanze kazi zake za uwindaji, vijiji vya jumuia hiyo havijanufaika .
Salum alisema kabla ya uwekezaji huo, jumuia hiyo ilikuwa ikipata mapato ya kati ya Sh milioni 200 na 300 kwa mwaka hivyo kufanya kila kijiji kupata mgawo wa Sh milioni 2.4 kila mwaka kwa ajili ya kufanya maendeleo na ulinzi.
Alisema kupitia fedha hizo walikuwa na uwezo wa kusomesha watoto wawili waliofaulu katika kila kijiji hivyo kufanya kila mwaka kusomesha wanafunzi 44.
Kwa mujibu wa mwanakijiji huyo, kutokana na mwekezaji huyo kutotoa mapato kwa vijiji, wamepoteza fursa za kusomesha watoto 210 wanaoingia kidato cha kwanza.
Vijiji vinavyounda Mbomipa ni Idodi, Ilolompya, Isele, Kinyika, Kisanga, Luganga, Mafuluto, Magozi, Mahuninga, Makifu, Mboliboli, Mkombilenga, Nyamahana, Itunundu, Kimande, Malizanga, Mbuyuni, Mapogoro, Kitisi na Magombwe.
Kinana aliahidi kushughulikia jambo hilo akisema: “Mkuu wa mkoa naomba nakala za barua mlizoziandika ili tukaulizane kwa nini waziri ukiandikiwa barua hujibu. Hii Serikali siyo mali mtu bali ni ya wananchi, lazima ajibu.”
Alisema tabia ya kujibu barua serikalini bado iko hovyo. Alikumbusha watumishi wa serikali kuwa utumishi serikalini ni wa wananchi kwa sababu serikali ni ya wananchi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Ilola Wilaya ya Iringa Vijijini, Kinana akawataka mawaziri ambao wameshindwa kutumikia wananchi na kutatua kero zao, wamweleze Rais Jakaya Kikwete waachie nafasi hizo.
Alikuwa akizungumzia mgogoro wa mipaka kati ya Magereza na vijiji ambao inadaiwa umeshindwa kutatuliwa na mamlaka husika.
“Hizi kazi tumezikubali za nini? kama kazi imekushinda, mwandikie bwana mkubwa (Rais Jakaya Kikwete), mwambie siwezi kazi yako. Wa kuchukua kazi hiyo wako wengi,” alisema.
Alisema pamoja na baadhi ya mawaziri kupelekewa barua za malalamiko ya migogoro ya wananchi, wanashindwa kwenda vijijini kutatua matatizo hayo, wakati ni wa kwanza kwenda Ulaya wanapopata mialiko ya huko.
 “Leo hii mawaziri wakipewa barua ya mwaliko kwenda Ulaya wa kwanza kwenda, akiandikiwa barua na Mkuu wa Mkoa kuwa wananchi wana mgogoro wa ardhi njoo, haji. Utasikia mbali, jua, vumbi, upepo,” alisema Kinana.
Aliongeza: “Anaandikiwa barua tatu na mkuu wa mkoa haji, hebu muulize amekwenda Ulaya mara ngapi tena wakati mwingine kwa mikutano ya porojo ambayo haina tija. Tutakwenda kushikana mashati.”
Kinana alisema viongozi hao wanatakiwa kujua kuwa kuna Watanzania ambao wako tayari kuwatumikia wananchi kwa hela ndogo
Alitolea mfano wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliotaka waongezewa posho za vikao kutoka Sh 300,000 hadi Sh 700,000 kwa siku wakati wapo walimu waliibuka na kumwambia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wako tayari kufanya kazi hiyo kwa Sh 40,000 kila siku.
Awali mwananchi kutoka Kisanga alimwomba Kinana kusaidia kutatua tatizo la mpaka kati ya kijiji hicho na Magereza ya Pawaga ambao umedumu kwa zaidi ya miaka sita.
Pia Mbunge wa Ismani, Lukuvi aliwataka wananchi hao kuacha kupoteza nauli kwenda kushughulikia suala hilo na kuwataka kuendelea kulima mpaka hapo wahusika watakapoona umuhimu wa kupima mipaka.
“Nimeshamwambia kamishna kuwa nimeshaamua, wananchi wa Kisanga wataendelea kulima eneo lile, haki ya ardhi ni ya yule anayelima sasa, mimi nipo na mwakani mtaendelea kulima mpaka hapo watakapozinduka na kuja kupima,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Ishengoma alisema walifanikiwa kutatua mgogoro wa vijiji vya Itunundu na Mbolimboli na kuwa mpaka wa Kisanga uliwawia vigumu hivyo kumwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani, aliyeelekeza kuwa Kamishina wa Magereza angefika kutatua tatizo hilo.
“Kamishina aliwahikufika hapa Iringa kwa shughuli zingine lakini hakuweza kufika katika eneo la mgogoro, hivyo mkoa bado unaendelea kufuatilia,” alisema.
Chanzo cha mgogoro ni gereza kupima na kuweka alama ya mipaka katika eneo la gereza ambalo vijiji vya Itunundu, Mbolimboli na Kisanga vilijikuta vikiwa ndani ya eneo la Gereza.

No comments: