KOMBANI ANUSURU AJIRA ZA DC, DEC MAABARA ZA 'KIKWETE'



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ametoa msaada muhimu wa Sh milioni 40 na bati 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule 12 za sekondari zilizopo katika jimbo la Ulanga Mashariki wilayani humo, mkoani Morogoro.
Mbali na msaada huo pia amesaidia vifaa mbalimbali ikiwamo sare, viatu na vyakula vyenye thamani ya Sh milioni 7.2 kwa askari wa jeshi la Mgambo wa wilaya ambao wanatumika kufyatua matofali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara.
Kombani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki alikabidhi misaada hiyo kwenye ziara yake aliyoianza jimboni humo jana, ambapo alisema ameamua kusaidia ujenzi huo wa maabara ili jimbo la Ulanga Mashariki liweze kutoa wanafunzi wenye utaalamu wa masomo ya sayansi katika siku za usoni.
Kutolewa kwa msaada huo kwa wilaya hiyo kunaweza kufanikisha utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mikoa wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule ya sekondari ya kata ifikapo Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa agizo la Rais, kiongozi yeyote katika ngazi za wilaya na mkoa kote nchini atakayeshindwa kutimiza wajibu kwa kutekeleza agizo hilo, atachukua maamuzi magumu dhidi yake.
Hata hivyo alisema, ili kufikia muda uliopangwa wa kukamilika kwa maabara hizo wameamua kuwatumia askari wa mgambo kwa ajili ya kutengeneza matofali na ujenzi huo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuleta maendeleo.
“Mimi nilishaanza kwa baadhi ya shule za jimboni mwangu  kujenga vyumba vya maabara kabla ya  agizo la rais, kwa hiyo huu ni mwendelezo na nia yangu ni kuhakikisha wana Ulanga wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo kwani dunia ya sasa ni sayansi na teknolojia,” alibainisha Waziri Kombani.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kwa kusema katika mafunzo yajayo ya mgambo atajitahidi  kuwapeleka  wakufunzi wa masuala ya ujasilimali ili wakati wanapata mafunzo pia wafundishwe namna ya kuendesha ujasilimali na sio ulinzi pekee ili waweze kujikwamua kwa kuongeza kipato.
Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya  hiyo, Isabela Chilumba, alisema  ujenzi wa vyumba vya maabara unaendelea na wananchi wameshahamasishwa kupitia mikutano mbalimbali kwa ajili ya kuchangia chochote ili  kukamilisha ujenzi huo.

No comments: