KIKWETE AONYA FEDHA ZA MAENDELEO KULIPA POSHO ZA MADIWANI



Rais Jakaya Kikwete amezitaka halmashauri nchini kuepukana na vishawishi vya kutumia fedha za maendeleo ya wananchi kulipia posho za vikao vya madiwani.
Rais Kikwete alisema hayo juzi wakati alipozungumza na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mwanza kwenye hafla ya uwekaji wa  jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Usagara-Kisesa kwa kiwango cha lami.
Rais amelazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kujulishwa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Mkoa wa Mwanza utapewa kiasi cha Sh bilioni 7.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mkoa huo ambao ziko chini ya Halmashauri za mkoa huo.
Fedha hizo kutoka Mfuko wa Barabara ni kiwango kikubwa zaidi cha fedha ambazo zimepata kutolewa kwa mkoa huo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za halmashauri ambazo haziko chini ya Wakala wa Barabara wa Tanroads.
“Fedha hizi ni nyingi. Kwa kweli kwa sasa, tatizo siyo upatikanaji wa fedha. Tatizo ni mchwa unaotafuna fedha hizi za umma. Kwa hiyo fedha hizo nyingi ambazo mnapewa msizitumie kulipia posho za madiwani. Jipangeni vizuri, zitumieni vizuri fedha hizo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ameweka  jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ya Usagara-Kisesa yenye urefu wa kilomita 16.95, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kikazi katika Mkoa wa Mwanza.
Barabara ya Usagara-Kisesa ambayo ni pamoja na ujenzi wa daraja kubwa la Nyanshishi inagharimu kiasi cha Sh bilioni 17.895 mbali na kiasi cha Sh 122 milioni ambacho kimetolewa na Serikali kufidia wananchi ambao mali zao zitaharibiwa kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara hiyo inalenga kurahisisha usafiri kati ya Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara na Kagera ambako sasa wasafiri hawatakuwa tena na ulazima wa kuingia katikati ya Jiji la Mwanza ili kuendelea na safari zao.
Ujenzi wa barabara hiyo unafanywa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works Limited na imepangwa kumalizika katika kipindi cha miezi 15.

No comments: