KACHERO WA KENYA ATOA USHAHIDI MAHAKAMANI DAR



Mkuu wa Uchunguzi wa Maandishi wa Jeshi la Polisi Kenya, John Kimani ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa saini zinazodaiwa kusainiwa na Ramadhani Balenga katika hati ya uhamishaji umiliki wa kiwanja pamoja na mkataba wa mauziano ni za kughushi.
Kimani alidai hayo katika mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kughushi inayomkabili Mkurugenzi wa Hoteli ya Rick Hill, Hans Macha.
Katika kesi hiyo, mfanyabiashara huyo anakabiliwa na mashitaka ya kughushi hati ya kiwanja chenye namba 183, Block A kilichopo Kigogo.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka, Kimani alidai alifanya uchunguzi baada ya Polisi nchini kumpelekea nyaraka, ikiwemo mkataba wa mauziano na nyaraka za uhamishaji umiliki wa kiwanja kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.
Aliieleza mahakama kuwa baada ya uchunguzi wao uliotumia vifaa vya utaalamu, walibaini kuwa saini zilizopo kwenye nyaraka hizo siyo za Balenga ni za kughushi.
Alidai wakati wanafanya uchunguzi walizingatia mambo mengi ikiwamo kuangalia mgandamizo wa kalamu, saini zote zilizokuwa na utata kwa kutumia kifaa maalumu.
Katika hatua nyingine, mpelelezi wa kesi hiyo, Inspekta Lugano Mwampeta alisema aliwahoji watu mbalimbali kuhusu jalada hilo, akiwemo Msajili wa Hati katika Ofisi ya Wizara ya Ardhi, na kubaini hati hiyo ina utata katika saini.
Aidha, alisema alifika katika eneo la kiwanja hicho ambacho kimejengwa ghorofa, na kugundua jengo hilo haliwezi kuuzwa kwa Sh milioni 20.
Hakimu Devotha, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushindi wa upande wa Jamhuri.

No comments: