Wakati kukiwa na matamanio na ushauri wa kutaka Rais Jakaya
Kikwete kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana kabla ya kuondoka madarakani, hatma
yake haijafahamika badala yake, suala
hilo imeachwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupatiwa
ufumbuzi.
Rais Jakaya Kikwete alisema jana kwamba kwa kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012
inatamka baada ya Katiba Inayopendekezwa
kukabidhiwa, kura ya maoni inatakiwa ifanyike ndani ya siku 84, jambo ambalo inabidi bunge lijalo
lifanye mabadiliko yatakayowezesha kura
ya maoni kufanyika baada ya uchaguzi mkuu.
Kikwete alisema hayo jana kwenye sherehe za kukabidhiwa
Katiba Inayopendekezwa zilizofanyika mjini Dodoma iliyokabidhiwa pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Rais ambaye kwenye sherehe hizo alieleza milima na mabonde
aliyokumbana nayo katika kuanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ,
alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka kuendesha kura ya maoni ndani ya
siku 84 kutoka tarehe ya rais kupokea katiba inayopendekezwa.
Hata hivyo alisema kulingana na maoni yaliyotokana na
mazungumzo kati yake na viongozi wa vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),
ilibainika muda ulibaki ni finyu na hautawezesha wala kutosha kukamilika kwa
shughuli hii kutokana na Tume ya Uchaguzi kutokamilisha mchakato wa daftari la
wapiga kura.
Alisema kutokana na maoni hayo, ilikubalika kushughulikia
mambo ya msingi ili kuwezesha uchaguzi
kufanyika na hatimaye Kura ya Maoni ufanyike baadaye.
“Inabadi sheria hii ipelekwe bunge lijalo kuruhusu
mabadiliko hayo. Maanake sasa ni siku 84. Nataka kusema Mwanasheria Mkuu
wanaangalia nini kinaweza kufanyika…mchakato unaendelea,” alisema Kikwete.
Aliendelea kusema, “Lakini pia wako watu wanasema tufanye
sasa kura ifanyike tumalize (alishangiliwa) lakini tume inasema wao wanaandika
daftari jipya na kazi inaisha Mei. Hapo ndipo penye mgogoro. “
Hata hivyo alisema wapo ambao wamekuwa wakimwambia kwamba
mbona mbunge akifariki, uchaguzi
hunafanyika na hivyo kuhoji kwa nini daftari linalotumika kwa ajili ya uchaguzi
huo mdogo, lisitumike kwa kura ya maoni. “Penye wengi pana mengi. Haya ndiyo yanaendelea kwenye tafakuri…”
ikifika mwisho wananchi watafahamishwa, “ alisema.
Miongoni mwa waliotamka bayana matamanio ya Kura ya Maoni
kupigwa kabla ya Rais Kikwete kutoka madarakani, ni pamoja na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda aliyetoa maoni hayo wakati wa kuhitimisha Bunge Maalumu la Katiba
.
Kauli hiyo ya Pinda iliyoungwa mkono na watu wengine akiwemo
mjumbe wa bunge hilo, Askofu Amos
Mhagache aliyesisitiza jana kwenye sherehe hizo, ilizua mjadala huku baadhi ya
watu wakiitafsiri kana kwamba ni uamuzi wa Serikali na hivyo kushutumu kuwa inapinganana
na makubaliano yaliyofikiwa kwenye.
Rais Kikwete ambaye alisisitiza kwamba tukio hilo la
kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa ni muhimu na la kihistoria linalokidhi
matakwa ya Sheria, alisema kukamilika
kwake kunabakiza hatua moja ya mwisho ya
wananchi wote kupiga kura ya maoni kufanya uamuzi wa katiba mpya.
“Tumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa hapa tulikofikia,…hakika Mungu anaipenda nchi yetu” alisema na
kushukuru u na kumpongeza Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu kwa kazi
waliyoifanya pamoja na wajumbe wengine kukamilisha kazi hiyo kwa kiwango cha
juu.
Alisema, “haikuwa kazi rahisi hata kidogo, kulikuwa na
milima na mabonde, na wakati mwingine
mawimbi ambayo yalikuwa makali yalielekea kuwa tufani.”
Alisema mchakato wa katiba mpya ni jambo o jema aliloanzisha
kwa nia njema ingawa lilipokewa kwa hisia tofauti. Alisema wapo walioona kwamba
halitawezekana lakini yeye alibaki kuwa mmoja wa walioamini kwamba litawezekana.
Kwa mujibu wake, Desemba 31, 2010 alipotangaza dhamira ya kuanza mchakato wa katiba,
ilipokewa kwa hisia tofauti; kwa maana
wapo waliunga mkono moja kwa moja, wapo waliopinga na waliobaki katikati.
Alisimulia, alisema
jambo ambalo wengi hawalifahamu, ni kwamba makundi hayo yalikuwepo pia ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nakumbuka walikuwepo baadhi ya watu waliodiriki hata
kulihoji na kuniambia kuwa wewe jambo hili umelizua wapi?...Hii si ajenda ya
CCM bali ni ya watu wengine.”
Alisema aliwaambia hiyo ni ajenda ya Watanzania na kwamba
yeye ndiye mwaklishi wao mkuu ambaye ana dhamana hiyo. “Nashukuru Mungu baada
ya mjadala mkali, tuakelewana,” alisema na kuendelea kusimulia kwamba, “walikuwepo pia watu
walioondoka pale shingo upande wakisema jamaa anaingiza jambo ambalo si letu.
Kwa mujibu wa Rais Kikwte, baadhi ya waliokuwa wakali kwenye
NEC na Kamati Kuu ya chama, aliwateua
kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu ambao hata
hivyo alisema anafurahi kwamba watu hao wamekuwa msaada mkubwa na kutooa mchango
mkubwa uliowezesha bunge kupendekeza katiba iliyo nzuri.
Alisema hatimaye wameelewa hoja na haja ya kuandika katiba
mpya ulioanza mwaka 2011 kwa serikali kuandaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ambao ulijadiliwa na kupitishwa Novemba 18, 2011.
Changamoto nyingine alizosema ni sintofahamu iliyojitokeza
kwenye Bunge ambayo baadhi ya wabunge walisusa wakitaka Rais asiridhie muswada wa sheria hadi hapo
yatakapofanyika marekebisho waliyoona wao ni muhimu.
Wakakubaliana kuwa kila chama kilete mapendekezo ya
marekebisho wanayoona yanafaa yafanyike. Wakawa na kamati ya pamoja kati ya
serikali na wao wakachambua moja baada ya jingine wakakubaliana kuwasilisha
kwenye bunge.
Akizungumzia mara nyingine ya baadhi ya wabunge (Ukawa)
kususa, Rais Kikwete wabunge waliobaki na hasa wengi wao wakiwa wa CCM ,
walikuwa wakimwambia safari hii asikutane nao, awaache kwamba kazi wataifanya
na kumaliza bila ya wao.
“Niliwasikiliza lakini nikafanya uamuzi wa kiuongozi; kwamba
lazima tufanye jitihada shughuli hii tuifanye wote tuimalize wote,” alisema.
Aidha alisema kutokana na mchakato wa bunge kukumbwa na
malumbano ya mara kwa mara, pia alikuwa akishauriwa ikiwemo kupokea meseji
nyingi zilizomtaka avunje Bunge Maalumu
la Katiba.
Rais meomba wananchi kupokea katiba inayopendekezwa akisema
ni nzuri hana wasiwasi nayo. “Tumefika mahali pa kuanza safari ya uamuzi wa
mwisho kwa kupiga kura.”
Alihadharisha wananchi
kwamba wataambiwa mengi kwa kuwa wapo wasemaji wengi. Aliwakumbusha kuzingatia msemo wa akili za
mbayu wayu wa kuchanganya akili za kuambiwa na zao.
Alisema anaamini
Katiba inayopendekezwa inafaa na katiba mpya iliyo nzuri inawezekana.
Alipongeza wajumbe kwa kutendea haki matarajio ya Watanzania
na kuwaambia kwamba majina yao yameandikwa kwa dhahabu kwa kutengeneza Katiba
inayojumuisha maslahi ya makundi yote na kuyajali.
Alitaja makundi hayo ni pamoja na wafugaji, wakulima, wazee,
wanawake. “Tangu dunia iumbwe, mfugaji
hajawahi kutajwa kwenye katiba yoyote ile,” alisema na kuongeza upande wa
wanawake kuwa katiba imesisitiza lazima 50 kwa 50 itekelezwe. Alisema hakuna nchi ya Afrika inayoifikia kwa
kuweka suala hilo kwenye katiba.
Katiba imependekeza mgawo mzuri wa mamlaka na madaraka
katika muungano. Orodha ya mambo ya muungano ni mpya, yale yote yaliyokuwa
yakituletea gozi gozi yameondoka…yamekuwa 16 na siyo 22,” alisema na kusisitiza
kwamba mambo yaliyokuwa na kero kubwa upande wa Zanzibari yamepatiwa majawabu.
Alieleza pia kuguswa na uwapo wa sura inayohusu ardhi,
maliasili na mazingira ambayo kwa mujibu wake, ndiyo mambo ya msingi ambayo
katiba isip0okuwa nayo kuna upungufu mkubwa.
Alisema katiba imekubaliwa kwa theluthi mbili kwa kila
upande jambo alilosema halikuwa rahisi hasa kwa upande wa Zanzibar ambayo
wajumbe siyo wengi.
Rais Kikwete ambaye alipongeza wadau mbalimbali ikiwemo Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, alisema, “natambua mengi yamesemwa baada ya
tume, katika warsha na makongamano, na mjadala naomba mkumbuke hekima ya
wahenga, yaliyopita si ndwele tugange yajayo. “
Alisema kila mwenye upande kwenye malumbano hayo, kama ingekuwa
ni vita, angesema sasa mapigano yasimamishwe.
Tume ilitimiza wajibu wake, Bunge la Katiba limemaliza
wajibu kilichobaki ni wananchi kupiga kura.
Pia alishukuru vyombo vya habari
akisema vimetoa mchango mkubwa wa mawazo kiasi cha mchakato kujulikana kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment