HALIMA MDEE NA WENZAKE WAACHIWA KWA DHAMANA


Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee (35) na wenzake wanane wameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 Mdee na wanachama wengine wanane waliachiwa jana mchana baada ya kutimiza masharti.
Masharti hayo yalikuwa kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni moja na kuwa na wadhamini wawili; mmoja awe mfanyakazi wa taasisi inayofahamika, awasilishe barua ya muajiri na kutambulisho cha kazi.
Baada ya kuachiwa, Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, alisema; “walifikiri kunilaza Segerea siku moja wamenikomesha, nimekula bata ambayo sijawahi kula, na walioamua kuficha barua za dhamana wajue kama tulikuwa tunachechemea sasa tunakimbia”.
Mdee na wenzake walifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa mashitaka mawili ya kutotii amri halali ya Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.
Walipelekwa rumande kwa kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa haujamaliza kukagua barua za wadhamini.
Washitakiwa hao wanadaiwa Oktoba 4, mwaka huu, katika mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali hao walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la  Polisi.
Katika mashitaka mengine, inadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, washitakiwa hao kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kutembea kwenda kwenye Ofisi ya Rais. Walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Rose Moshi (45), Renina Peter maarufu kama Lufyagila, Anna Linjewile (48), Mwanne Kassim (32), Sophia F angel (28), Edward Julius (25), Martha Mtiko (27) na Beatu Mmari (35).
Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na itatajwa tena Oktoba 21 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

No comments: