Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba,
Andrew Chenge amesema
asilimia 81.8 ya mapendekezo ya rasimu iliyowasilishwa
bungeni na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yamo katika Katiba mpya
Inayopendekezwa.
Chenge aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akitoa
maelezo kuhusu uandishi wa
rasimu hiyo ya mwisho ya mapendekezo ya Katiba kwa Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk Mohammed Shein.
Chenge aliyataja maeneo makubwa matatu ambayo rasimu ya
mwisho ya Katiba
Inayopendekezwa imeyazingatia kuwa ni muundo wa Muungano,
upungufu wa baadhi ya
mambo katika rasimu ya Tume na maboresho na marekebisho ya
taaluma ya uandishi na
maneno katika baadhi ya ibara.
Akizungumzia Katiba mpya kuwa na mambo mengi
yaliyopendekezwa na wananchi kupitia
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Chenge alisema
asilimia 81.8 ya maoni ya
wananchi kama walivyopendekeza kwenye Tume hiyo iliyokuwa
chini ya Jaji Joseph
Warioba yamechukuliwa. Alisema Ibara 46 ambazo ni sawa na
asilimia 10.7 zimefutwa na
Ibara 54 sawa na asilimia 18.2 ni mpya.
Kuhusu mabadiliko ya muundo wa serikali, Chenge alisema
kutakuwa na Serikali mbili
na kwa mara ya kwanza sasa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itakuwa na Rais na
Makamu watatu wa Rais, ambao watatokana na mgombea mwenza
atakayekuwa Makamu wa
Kwanza wa Rais, Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa
Rais na Waziri Mkuu
atakuwa Makamu wa Tatu wa Rais.
Alisema pia Katiba hiyo Inayopendekezwa imeweka ukomo wa
idadi ya mawaziri ambapo
sasa kutakuwa na Mawaziri na Naibu Mawaziri 40 tu, hatua
itakayoipunguzia serikali
mzigo. Alisema Bunge pia litaundwa kwa kuzingatia uwiano na
ukomo wa idadi ambapo
uwiano sasa utakuwa asilimia 50 kwa 50 kwa wanaume na
wanawake na ukomo wa idadi
itakuwa wabunge kati ya 340 na 390.
Alisema ili kukidhi muundo huo mpya wa serikali ambao
ulitofautiana na ule wa Tume
iliyopendekeza muundo wa serikali tatu, baadhi ya ibara
ziliongezwa na nyingine
kufutwa, kuboreshwa au kubadilishwa ili kukidhi muundo mpya
wa serikali na ibara
zilizoathirika zaidi ni
Ibara ya Kwanza na Sita ya Rasimu ya Tume.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, Rasimu ya Mwisho ya
Katiba Inayopendekezwa
ambayo sasa itapelekwa kwa wananchi ili kupigiwa kura
itakuwa na sura 19 zenye ibara
296 tofauti na ile ya Tume iliyokuwa na Sura 17 na Ibara
271.
"Mheshimiwa Rais, Bunge lilijadili rasimu ya Tume
kupitia Kamati 12, ambapo mjadala
ulijielekeza katika kuboresha, kurekebisha, kupunguza na
kuongeza ibara mpya kwa
kadri ilivyoonekana inafaa lakini rasimu ya Warioba ndio
ilikuwa msingi wa mjadala,"
alisema Chenge.
Alisema Katiba inayopendekezwa imezingatia mambo muhimu
mapya yakiwemo muundo wa
serikali, utawala bora, haki za binadamu lakini pia uhuru
kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kuanzisha uhusiano na taasisi yoyote ya kikanda
au ya kimataifa kwa
masuala yanayoihusu Zanzibar.
Alisema mambo mengine mapya yaliyozingatiwa kwenye rasimu ya
mwisho ya Katiba
Inayopendekezwa ni
suala la utafiti wa maendeleo, dira ya taifa ya maendeleo na
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya taifa, lengo likiwa ni
kuhakikisha kuwa
rasilimali za nchi ikiwemo madini, mafuta na gesi
zinalinufaisha taifa na Watanzania
kwa ujumla.
Kuhusu mambo yaliyotajwa na Tume kuwa ni Tunu za Taifa,
Chenge alisema Bunge Maalum
la Katiba limeyaondoa mambo hayo ambayo ni uwazi,
uwajibikaji, demokrasia, utawala
bora, utawala wa sheria, uzalendo, haki za binadamu na usawa
wa kijinsia kutoka kuwa
tunu za taifa na kuwa misingi ya taifa.
No comments:
Post a Comment