YONA KUANZA KUJITETEA MATUMIZI MABAYA YA OFISI


Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona leo anaanza kujitetea mahakamani dhidi ya tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. 
Yona pamoja na aliyekuwa  Waziri wa Fedha, Basil Mramba na  Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. 
Jopo la mahakimu Sam Rumanyika, John Utamwa na Saul Kinemela liliamuru Yona na Mgonja waanze kujitetea kwa kuwa mashahidi wa Mramba hawawezi kupatikana kwa sasa na kesi hiyo ni ya muda mrefu. 
Awali Wakili wa Mramba, Peter Swai aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa sababu mashahidi wa Mramba hawakufika mahakamani kwa kuwa wengine wako kwenye Bunge Maalumu la Katiba. 
Mashahidi hao ni Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo, Kalisti Elias kutoka Wizara ya Fedha na Yusto Tongola. 
Yona, Mramba na Mgonja wanadaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. 
Ilidaiwa walisababisha hasara hiyo baada ya kutoa msamaha wa kodi kinyume cha sheria kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

No comments: