WASIMAMIZI WA MITIHANI DARASA LA SABA WAONYWAWizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  imewataka wasimamizi wa mitihani ya darasa la saba unaotarajiwa kufanyika leo kufanya kazi kwa umakini na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa na kueleza kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Alisema Serikali itachukua hatua kali kwa msimamizi yeyote atakayegundulika kujihusisha na udanganyifu wowote au kukiuka utaratibu katika kipindi chote cha usimamizi.
Kwa mujibu wa Mhagama, watahiniwa 808,111 wanatarajia kufanya mtihani huo. Wavulana ni 378,470 sawa na asilimia 46.84 na wasichana ni 429,641 sawa na asilimia 53.16. Watafanya jumla ya mitihani mitano Kiswahili, Kingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Aidha alisema watahiniwa 783,223 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na 24,888 watafanya kwa Kiingereza ambayo ndio lugha waliyokuwa wakitumia katika kujifunzia katika elimu ya msingi.
Pia alisema wapo watahiniwa 86 wasioona walioandikishwa kufanya mtihani, wavulana ni 54 na wasichana ni 32 huku watahiniwa wenye uono hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa wapo 714, wavulana 371 na wasichana 343.

No comments: