WANAFUNZI WA KIKE WANUSURIKA KUFA KWA MOTO



Zaidi ya wanafunzi 96 wa kike wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari African Muslim iliyopo mjini Moshi, wamenusurika kifo baada ya bweni walilokuwa wakilala, kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana mjini hapa.
Moto huo ambao bado chanzo chake halisi hakijajulikana, ulianza saa 7:45 usiku, ulidumu kwa zaidi ya saa tano, ukianzia katika choo cha shule hiyo jirani na Bweni la Makka.
Baadaye moto huo uliunguza  chumba kinachofuata na kusambaa kwenye vyumba 20 vilivyoko katika bweni hilo lenye ghorofa moja.
Mkurugenzi wa Shule hiyo, Ali Adam Ali, alisema  katika tukio hilo wanafunzi wanne walipoteza fahamu kwa hofu na kukimbizwa hospitali na sasa hali zao ni nzuri huku wanafunzi wengine wa Kidato cha Pili na Nne wakijitahidi kuokoa baadhi ya mali zao.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema wanafunzi hao walikuwa hawajaingia kulala na wakati huo walikuwa wakijiandaa kwa sala ya Isha ambapo mmoja wa wanafunzi aliwajulisha wenzake juu ya kuhisi harufu kali ya moshi na baadaye kutoa taarifa za kuwapo kwa moto huo.
Ali alisema moto huo umesababisha hasara ya mamilioni ya shilingi kwani wanafunzi hao walipoteza baadhi ya vitu vyao ikiwamo vitabu, vitanda na nguo.
Ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Manispaa ya Moshi.
Miongoni mwa viongozi waliofika shuleni hapo ni pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ikiongozwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Ibrahim Msengi.
Msengi aliagiza uongozi wa shule hiyo kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kufanya tathimni ya hasara iliyopatikana.
Aidha katika agizo hilo, Dk Msengi alimtaka Mkurugenzi wa shule kufuatilia kwa makini chanzo cha moto huo na kuwasilisha taarifa mezani kwake mapema iwezekanavyo.
Wakati huo huo, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Estomih Makyara amemtaka Mkurugenzi wa shule hiyo kutoa wiki moja ya mapumziko kwa wanafunzi walioathirika na moto huo.

No comments: