Raia wa China waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuvua samaki
kinyume cha sheria, wamewasilisha barua
kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kutaka warudishiwe Meli ya
Tawariq 1 na samaki waliopokewa mahakamani kama vielelezo.
Barua hiyo iliwasilishwa na kampuni ya uwakili ya M and B iliyokuwa ikiwawakilisha Wachina
hao na kusaini na mshirika wa kampuni
hiyo, Ibrahim Bendera.
Katika barua hiyo, raia hao wanaiomba mahakama iwarudishie
meli hiyo pamoja na tani 296.3 za samaki zenye thamani ya Sh bilioni 2.074 ambazo zilipokelewa mahakamani
hapo kama vielelezo katika kesi namba 38/2009 iliyokuwa inawakabili.
Hatua hiyo inatokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu iliyotolewa na Hakimu Mfawidhi Isaya Arufani Agosti 23, mwaka huu wakati
akiwaachia huru washitakiwa wawili; nahodha wa meli hiyo, Hsu Chin Tai na
wakala wa meli, Zhao Hanquing.
Awali watu 35 kutoka mataifa mbalimbali walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye kesi hiyo ilihamishiwa katika
Mahakama Kuu mbele ya Jaji Razia Sheikh ambaye alipokea vielelezo hivyo.
Kesi hiyo ilihamishiwa kwa Jaji Augustino Mwarija, ambaye
aliwaachia huru washitakiwa 31 na kuwahukumu
Tai na Hanquing kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya Sh bilioni
22. Hata hivyo mmoja wa washitakiwa alifariki dunia wakati kesi hiyo
ikiendelea.
Washitakiwa hao walikata rufaa kupinga adhabu hiyo. Machi
28, mwaka huu, Mahakama ya Rufani iliwaachia huru kabla ya kukamatwa tena na
kufunguliwa upya mashitaka hayo.
Wakati kesi hiyo
ikiendelea, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), aliwasilisha hati ya kutokuwa na nia
ya kuendelea kuwashitaki. Aliwaachia huru na Mahakama kuamuru warudishiwe mali
zao.
Washitakiwa walikamatwa wakati Dk John Magufuli akiwa Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, hali iliyochangia samaki waliokamatwa kuitwa
wa 'Magufuli’ hasa baada ya serikali kuamua kutaifisha meli na pia kugawa
samaki kwa wananchi, vyuo na taasisi nyingine za umma.
No comments:
Post a Comment