Baadhi ya
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamesema wala rushwa pamoja na wahujumu
uchumi adhabu yao iwe ni kunyongwa.
Wametaka Katiba mpya inayoenda kuandikwa itamke hivyo
ili kufanya viongozi wa kisiasa kuogopa kama ilivyo kwenye nchi nyingine.
Sababu ya
wajumbe hao kupendekeza jambo hilo ni kwamba uhujumu uchumi na rushwa nchini
limekuwa tatizo kubwa kwa viongozi.
Kutokana na
ukiukwaji huo wa maadili, wamesema
umefika wakati wa kuweka bayana suala hilo kwenye sheria mama.
Miongoni mwa
waliochangia ni Paul Makonda aliyesema
suala hilo likiwekwa bayana, litaokoa fedha nyingi za walipa kodi ambazo kwa
sasa baadhi ya viongozi wanazichota na kwenda kuzihifadhi nje ya nchi.
Pia alipinga
kuruhusu viongozi wa nchi kufungua akaunti nje ya nchi. “Kwa nini viongozi hao
washindwe kuhifadhi fedha zao ndani ya nchi, wanafanya biashara gani hadi
wakafungue benki nje ya nchi?
“Tusiruhusu
jambo hili na napendekeza kwamba kiongozi atakayebainika amekula rushwa na
kuhujumu uchumi huyo anyongwe,” alisema Makonda.
Yusuf Singo
pia alisema maadili yanazidi kuporomoka kwa viongozi, jambo linalorudisha nchi nyuma. Alitaka
Katiba isisitize maadili kwa kada hiyo na ambao watakiuka wanyongwe.
Alitoa mfano
wa Japan kuwa kiongozi wa kisiasa anapochunguzwa kwa kujihusisha na rushwa
anatoa machozi kwa sababu hajui hatima yake. “Tunataka na sisi ifike wakati
kiongozi akianza kuchunguzwa atoe machozi,” alisema.
Dk Mary
Mwanjelwa katika mchango wake alisema rushwa imekuwa adui mkubwa wa maendeleo
ya Watanzania. Alisema isipopingwa kuanzia kwenye Katiba, nchi itakuwa
inajichora.
Alisema Bunge
halitaeleweka kama halitaweka jambo hilo kwenye Katiba, kwa sababu wananchi
wengi wameteseka ndani ya nchi yao kwa sababu ya rushwa.
Alisema pia
wapo viongozi wengi wasio na maadili na
ndiyo maana wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
Kwa upande
wake, Profesa Mark Mwandosya alisema tatizo la rushwa haliwezi kutenganishwa na
haki za binadamu kutokana na kukosesha wananchi maendeleo.
Profesa
Mwandosya alisema Katiba lazima itambue adui wa haki za wananchi ni rushwa.
Alipendekeza
suala hilo litambulike kikatiba na serikali zote mbili zitunge sheria kali za
kupambana na rushwa kuhakikisha wananchi
wanapata haki zao za msingi bila kutoa wala kupokea rushwa.
Naye Gerison
Lwenge alisema Katiba itambue jambo hilo
na ikemee vikali kwa wanaotoa na wale wanaopokea.
Alisema kwa
ahli ilivyo, wanaobanwa zaidi ni wale ambao wanapokea na akapendekeza sheria
kali zitungwe kubana pia wanaotoa.
Alishauri
Kamisheni isimamie suala hilo la rushwa badala ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kwa mujibu wa
Lwenge, Kamisheni ni chombo kikubwa zaidi kuliko ilivyo kwa taasisi. Alisema
kazi yake itakuwa ni kuzuia zaidi na si
kutibu pekee.
Jesca
Msambatavangu alisema Takukuru wanafanya kazi vizuri na walishindwa kupambana
na rushwa kwa vile hawana uhuru wa kutosha.
Alisema kama
Takukuru wakipewa meno kupitia Katiba mpya, watashughulika kwa uhuru zaidi
katika kupambana na tatizo la rushwa nchini.
No comments:
Post a Comment