UTULIVU WATAWALA MITIHANI DARASA LA SABA



Wanafunzi wa darasa la saba mkoani hapa wamefanya mitihani yao ya kuhitimu elimu hiyo kwa utulivu na usalama mkubwa kutokana na kuwepo kwa maandalizi ya kutosha.
Ofisa Elimu wa Mkoa, Raymond Mapunda alisema hayo jana wakati akizungumza na HabariLeo na kuongeza kuwa mtihani huo umefanyika katika shule 511 katika hali ya amani na utulivu huku kukiwa na ulinzi katika maeneo yote.
Alisema wanafunzi 60,710 ndio walioandikishwa kwa ajili ya kufanya mtihani huo na kila chumba cha mtihani chenye wanafunzi 25 kitakuwa na msimamizi mmoja.
“Tunategemea mtihani kumalizika kwa amani bila kuwepo kwa udanganyifu wowote… kwani maandalizi yalikuwa mazuri na ya kutosha yakitegemewa kuwa na ufaulu mkubwa,” alisema Mapunda.
Kuhusu usimamizi katika chumba cha mtihani alisema ni walimu waliopewa mafunzo maalumu na kwamba hawatoki katika shule wanazozisimamia.
Mapunda alisema kwa siku ya jana wanafunzi hao walifanya mitihani ya  Hisabati, Sayansi na Kiswahili.
Kuhusu mategemeo ya Mkoa alisema wanatarajia kuwepo kwa matokeo mazuri kutokana na kwamba tangu mwaka ulipoanza hapajakuwepo kwa migomo au migogoro ya walimu ambayo ingesababisha kuonekana kama ufundishaji haukukidhi matakwa stahiki.
Kuhusu vifaa katika vyumba vya mitihani alisema hali ni shwari na hadi wanafunzi hao wanafanya mtihani wao wa tatu, ofisi yake haikupata malalamiko yoyote yenye kuhusiana na upungufu.
Akizungumzia mtihani huo juzi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema watahiniwa 808,111 wanatarajiwa kufanya mtihani huo.
Wavulana ni 378,470 sawa na asilimia 46.84 na wasichana ni 429,641 sawa na asilimia 53.16 ambao watafanya mitihani mitano ya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya jamii.

No comments: