Sekta
ya Utalii nchini imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa
mwaka jana ilichangia dola bilioni 1.8 (Sh trilioni 3) katika pato hilo.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi alisema
hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
Onesho la Kimataifa la Utalii (SITE).
Alisema
sekta hiyo imekuwa na mchango mkubwa. Alisema kutokana na ukuaji wake, wameamua
kuanzisha onesho hilo, ambalo litakuwa likifanyika kila mwaka.
“Kwa
mwaka huu maonesho hilo kubwa la kimataifa litafanyika kuanzia Oktoba mosi hadi
nne ambapo watakuwepo wageni kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kutangaza
utalii,” alisema.
Alisema
katika kufanikisha maonesho hayo, wamewashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo
TANAPA, Hifadhi ya Ngorongoro, Kampuni ya ndege ya Ethiopia, makampuni na
mashirika mengine, ambapo TTB imechangia Sh milioni 500 katika maandalizi hayo.
Alitoa
mwito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza
utalii wa ndani na kujivunia vivutio vilivyopo na kutafuta soko kupitia
wadau walioalikwa katika maonesho hayo.
Mratibu
Mkuu wa maonesho hayo, Philip Chitaunga alisema lengo la maonesho hayo ni
kuwakutanisha watanzania na masoko ya nje na pia watawaleta wadau mbalimbali
wanaoandika habari za utalii na wadau wenye makampuni ya watalii.
Wageni hao pia watapata fursa ya kufanya
ziara kwenye vivutio mbalimbali, ikiwemo Zanzibar na Ngorongoro, ambapo kwa
watanzania itakuwa ni fursa kwa wenye makampuni ya watalii kujitangaza na
kutafuta soko.
No comments:
Post a Comment