TIGO WAANZA KUTOA GAWIO KWA WATEJA WAKE



Katika kuhamasisha utunzaji wa fedha ulio salama hasa kwa wakazi wa vijijini, Kampuni ya simu za mkono ya Tigo imeanza kutoa gawio la faida kwa wateja wake wanaoweka fedha zao katika Tigo-Pesa kama ambavyo hutolewa na benki.
Huduma hiyo inawafanya wananchi kupata gawio la faida katika fedha wanazotunza kila baada ya miezi mitatu ambapo jana, kwa mujibu wa Tigo, mteja atatakiwa kutuma ujumbe mfupi wa neno “Wekeza” kwenda nambari 15514 na kupata maelekezo ya gawiwo lake na baadaye kutumiwa.
Huduma hiyo imetangazwa jana na Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez ambaye alisema zaidi ya wateja milioni 3.5 wa Tigo Pesa watanufaika na malipo hayo ambayo yatatolewa mara nne kwa mwaka yaani kila baada ya miezi mitatu.
“Hii ina maana ya kwamba Tigo Pesa haitakuwa tena huduma ya kutuma na kupokea pesa tu kama ilivyo hivi sasa bali ni njia mojawapo kujipatia kipato cha ziada kupitia huduma ya Tigo Wekeza,” alisema Gutierrez.
Wiki iliyopita, Tigo ilitangaza kutoa gawio la Sh bilioni 14.25 kwa wateja wake wa Tigo Pesa kutoka katika mfuko wa fedha ya akaunti ya Tigo Pesa, kitendo kilichoifanya kuwa kampuni ya simu ya kwanza duniani kutoa gawiwo kupitia huduma ya kutuma na kupokea fedha. Gawio hilo liliidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Julai mwaka huu.
“Tunatarajia kuona ongezeko la faida kutokana na uzinduzi huu wa huduma ya Tigo Wekeza ambayo tunaamini itakuwa kichocheo kwa wateja wengi zaidi kujiunga na kuanza kutumia Tigo Pesa kama sehemu ya kuhifadhi pesa zao pamoja na kutengeneza kipato, tunatarajia kuona ongezeko la Watanzania kujiunga na mfumo wa fedha kitaifa,” alisema Meneja Mkuu huyo.

No comments: