MWANAMKE AANGUKA KWENYE BODABODA NA KUKANYAGWA NA GARIMwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 amekufa papo hapo baada ya kudondoka kwenye pikipiki aliyokuwa amepanda na kisha kukanyagwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi mchana katika barabara ya Bagamoyo eneo la Tangibovu ambapo gari likiendeshwa na dereva asiyefahamika akitoka kwa Alysykes kuingia barabara ya Bagamoyo, aliigonga pikipiki namba T 505 CTJ Fekon ikiendeshwa na dereva asiyefahamika.
Alisema pikipiki hiyo iliyokuwa ikitokea Mbezi Makonde kwenda Mwenge ilikuwa imempakia mwanamke huyo ambaye baada ya pikipiki kugongwa alianguka chini na kisha kukanyagwa na lori namba T 277 CIL aina ya Tata likiwa na trela namba T 339 CYB lililokuwa katika uelekeo mmoja na pikipiki.
Kamanda alisema mwanamke huyo alikufa papo hapo na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala huku Polisi wakiendelea kuwasaka madereva waliohusika katika ajali hiyo.
Wakati huo huo moto umezuka katika baa ya Elements iliyopo maeneo ya Masaki na kuteketeza eneo la jikoni na mali zote zilizokuwamo ndani. Thamani bado haijajulikana na haukuwa na madhara kwa binadamu.

No comments: