MWAKYEMBE AJIVUNIA KUFUFUA TRL, KUPOKEA MABEHEMU 3,345Moja ya mafanikio ya wazi ya Serikali ya Awamu ya Nne katika usafirishaji, ni kufufuliwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRL), ambalo lilikuwa limekufa na kupoteza uwezo wake wa kiuendeshaji.
Akizungumza katika semina ya madereva wa treni mkoani Dodoma jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alieleza namna shirika hilo lilivyokuwa hoi mwaka jana na kufafanua kazi iliyofanyika kwa muda mfupi kulifufua na matarajio yake.
Alisema TRL ilikuwa hoi kioperesheni, baada ya kuanguka kutoka kuwa na vichwa vizima vya treni zaidi ya 50 mwaka 2002, hadi kubakiwa na vichwa vinane tu mwaka 2013.
Hali hiyo ya kuporomoka kiuendeshaji kwa shirika hilo, kuliathiri hata usafirishaji wa mizigo ambapo Waziri Mwakyembe alisema ubebaji wa mizigo kwa mwaka ulikuwa tani milioni 1.5, mwaka 2002 ukashuka mpaka tani 155,000 mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Waziri Mwakyembe, Serikali imefanya kazi kubwa ya kuimarisha njia ambapo mpaka sasa wamekarabati karibu kilometa 600 za reli.
Aidha, alisema kazi ya ufufuaji wa injini za treni, imeanza na kati ya injini nane walizopeleka karakana ya Morogoro kwa ajili ya kujengwa upya, injini saba zipo tayari na ya nane inakamilika mwezi huu.
Katika mabehewa, alisema kazi kubwa imefanyika hasa katika kupata mabehewa mapya ya abiria na mizigo, ambapo mengine yamefanyiwa ukarabati mkubwa hapa nchini na mwaka huu wanatarajia kupokea mabehewa 356 ya mizigo na abiria.
Pamoja na mafanikio hayo, Dk Mwakyembe alisema bado mahitaji halisi wanayopigania ni kufikia vichwa 102 vya treni na mabehewa 3,345 ya mizigo na abiria.
Akielezea changamoto zilizopo katika ufufuaji wa shirika hilo,  Waziri Mwakyembe alisema kumeibuka tabia ya wizi wa
mafuta pamoja na matumizi mabaya ya mali za shirika hilo.
Alitaja tabia hizo kuwa ni wizi wa mafuta, kutokuwa waaminifu katika kuendesha vichwa vya treni pamoja na mabehewa, jambo
linalosababisha kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mali za Serikali.
Mwakyembe alisema amekuwa akivunjika moyo pale anapoona wafanyakazi wanaendelea na tabia zile zile za kubomoa Shirika, licha ya juhudi hizo za wazi za Serikali katika kulifufua.
Alisema ni vigumu kwa Serikali kuanza kuboresha hali za
wafanyakazi katika mazingira ya udokozi, wizi, ubadhirifu na uzembe.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mwakyembe aliwatangazia ‘vita’ madereva wa treni, ambao watabainika kuiba mafuta au kutumia vibaya mali ya shirika hilo.
Alisema Serikali haiwezi kuvumilia madereva watakaofanya makusudi kuiba mafuta, kutokuwa makini katika utumiaji wa vichwa vya treni au mabehewa, kwani watawajibishwa bila kuwa na huruma.
“Hakuna dereva atakayeonewa aibu pale atakapobainika kuhusika katika uharibifu wa mali za TRL kwani pamoja na Serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika shirika, bado kuna watumishi wanaendeleza tabia mbaya,” alionya.
Pamoja na mafanikio na tahadhari waliyopewa watendaji hao wa TRL, madereva hao walilalamikia shirika hilo kwa kuwa na maslahi duni kuliko hata madereva wa daladala.
Mmoja wa madereva hao, Adolf Mwabugale alisema maisha ya madereva wa treni yamekuwa magumu zaidi kutokana na shirika kutowathamini kwa kuwaongezea maslahi.
Mwabugale alisema inasikitisha kuona madereva wanaosafirisha mizigo yenye thamani kubwa pamoja na kuwa na ulinzi mkubwa wa treni, lakini maisha yao ni mabaya zaidi kuliko wafanyakazi wengine serikalini.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mwakyembe alisema pamoja na kuwepo kwa vitendo vya wizi wa mafuta kwa madereva, bado serikali imeweka utaratibu wa kuboresha maisha ya madereva wa treni, ambao watafikisha mizigo yao vizuri katika vituo vyao.
Mwishoni mwa Julai mwaka huu, Waziri Mwakyembe alipokuwa akipokeamabehewa 25 yenye thamani ya Sh bilioni 4.3 kutoka India, alisema mabehewa hayo ni sehemu ya mpango kabambe wa Serikali wa kufufua TRL chini ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Katika mapokezi hayo, Mwakyembe alisema chini ya BRN inayoratibiwa na Ofisi ya Rais, Serikali imelenga kuwezesha shirika hilo kiutendaji, ili lifanikishe kusafirisha tani milioni 3  ifikapo 2016 kutoka tani 200,000 zilizokuwa zikisafirishwa mwaka 2012 kupitia Reli ya Kati.
"Katika harakati za kufikia malengo haya makubwa, Serikali kupitia bajeti zake za mwaka 2012/13 na 2014, ilitenga fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali iliyolenga kuboresha vitendea kazi vya TRL," alisema Mwakyembe katika mapokezi hayo ya mabehewa mapya.

No comments: