MV KIGAMBONI KUANZA TENA KUTOA HUDUMA KESHO



Kivuko cha Mv Kigamboni kilichokuwa kwenye matengenezo, kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kesho na Serikali imeokoa zaidi ya Sh milioni 300 kwa kufanya matengenezo hayo hapa nchini.
Sambamba na hilo, Serikali imesema kivuko kipya cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo kinatarajiwa kuingia nchini baada ya wiki nne na kitasaidia kupunguza foleni ya Jiji la Dar es Salaam. Kivuko hicho kilitengenezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark kwa gharama ya Sh bilioni 7.9.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alipotembelea eneo kinapofanyiwa matengenezo na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kamandi ya Maji.
Alisema matengenezo yaliyofanywa na jeshi hilo, yameokoa zaidi ya nusu ya fedha iliyokuwa imekadiriwa kukarabati kivuko hicho Mombasa nchini Kenya, ambapo makadirio yake yalikuwa zaidi ya Sh milioni 600.
 “Natoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na JWTZ ukiwemo ukarabati wa kivuko hiki, ni kweli kivuko tungekipeleka nje gharama ya matengenezo ingekuwa kubwa kuliko ilivyo sasa na pia tusingekuwa na uhakika kama wananchi wangeweza kukitumia wiki hii kwa kuwa kingechukua muda mrefu ila nyie mmefanya kazi kwa moyo wa kizalendo,” alisema.
Alisema kazi waliyoifanya wanajeshi hao ni kubwa na kutoa mwito kwa taasisi nyingine, kutokimbilia watu wa nje kufanya kazi zao, badala yake watoe fursa kwa Watanzania kwanza kwa kuwa nao wanaweza.
“Nawaahidi kivuko cha Mv Kigamboni kikirudi mjipange tena kwa sababu tutawaletea Kivuko cha Mv Magogoni nacho mkifanyie matengenezo kwa kuwa muda wake umewadia. Nataka hata kama kuna kushindanishwa nyie ndiyo mshinde kwa kuwa mmefanya kazi nzuri na pia nyie siyo wezi,” alisema.
Alisema “kama kivuko hicho kingetengenezwa huko nje usalama na ubora wake ungekuwa wa mashaka kwa sababu hata tusingepata muda wa kuja kukitembelea na kukagua kazi inavyoendelea kama tunavyofanya sasa na hata tungetuma watu  pengine nao wangeongea nao vizuri”.
Aliwaomba wanajeshi hao kuingiza kivuko hicho kwenye maji leo jioni ili wananchi wa Kigamboni wakitumie kesho kwa sababu kazi kubwa imemalizika na kilichobaki ni kumalizia mambo madogo ikiwemo kupaka  rangi.
Alisema Wizara yake itaendelea kutumia utaalamu wa jeshi hilo katika kazi zake na kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri,  Dk Magufuli alitoa ng’ombe wawili kwa ajili ya mafundi hao kusherehekea kazi waliyoifanya.
Kuhusu kivuko kipya cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, alisema kinatarajiwa kuingia nchini kutoka Denmark baada ya wiki chache.
“Tuliahidi kuwa kitakuja kivuko kipya cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo kupunguza msongamano, leo hii kimeingia majini huko na baada ya wiki tatu hadi nne kitakuwa kimeshafika nchini,” alisema Magufuli.
Awali, Mkuu wa Kamandi hiyo, Brigedia Jenerali Rogastian Laswai alisema mafundi walioshiriki katika matengenezo hayo ni 55, wakiwemo wahandisi, mafundi mchundo na vibarua.

No comments: