Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imesema usajili wa
pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ utafanywa pamoja na kukagua namba zenye rangi
ya njano huku zikiwa zinafanya biashara, jambo ambalo ni kinyume.
Meneja
Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray
alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na HabariLeo kuhusu usajili wa namba za pikipiki
pamoja na zenye magurudumu matatu ili ufanywe pamoja na kukagua rangi
zinazotakiwa kwa biashara.
Usajili wa
namba za pikipiki na zenye magurudumu matatu unatarajiwa kufanywa na Mamlaka ya
Mapato nchini (TRA) ambapo namba zote zitabadilishwa kuanzia Oktoba mosi.
Akizungumzia
usajili huo, Mziray alisema kimsingi kazi hiyo itafanywa na TRA lakini Mamlaka
hiyo inaiomba Mamlaka ya Mapato kuendesha usajili pamoja na ukaguzi wa rangi za
namba za pikipiki.
“Zipo
bodaboda nyingi ambazo zina rangi za njano na ambazo zinaendelea kutoa huduma
kibiashara wakati rangi inayotakiwa ni
nyeupe…tumewaambia TRA wakati wa usajili huo wakague pia,” alisema
Mziray.
Alisema
wamiliki wengi wa pikipiki wanapoagiza vifaa hivyo wakati wa kuvitoa bandarini
hudanganya kana kwamba sio vya biashara ili kukwepa kulipa kodi lakini baadae
huonekana mitaani vikifanya kazi kibiashara.
Alisema
kutokana na usajili huo kufanywa na TRA, Mamlaka ya Sumatra itafanya ukaguzi
huo ili kupunguza mianya ya wasiolipa kodi.
Kuhusu
usajili huo, taarifa ya Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi ilifafanua kuwa
TRA inawataka wamiliki wote wa vifaa hivyo kuwa mfumo mpya wa usajili wa namba
za pikipiki unaoanzia namba MC 101 AAA badala ya namba zinazotumika sasa.
“Kwa mantiki
hiyo wamiliki wote namba zote zitabadilishwa kuanzia Oktoba mosi, hivyo wafike
katika ofisi za TRA kwa ajili ya kazi hiyo,” alieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo, kazi ya ubadilishaji wa namba hizo utafanywa bila adhabu kwa
kipindi cha miezi sita kuanzia Oktoba mosi mpaka Machi 31, mwakani na baada ya
muda huo ubadilishwaji utafanywa na adhabu.
No comments:
Post a Comment