Wafanyabiashara ndogo (wamachinga) wamedai hatua ya
kuondolewa katika maeneo mbalimbali ya jiji
wasifanye biashara, huenda ikachukua muda mrefu kufanikiwa, kwa kile
walichodai wana ‘mikataba’ maalumu na mgambo
wa jiji.
Baadhi ya wafanyabiashara hao, walisema ni vigumu kuwaondoa
kwani wana makubaliano maalumu ya malipo ya kila siku kati yao na mgambo na
utaratibu wa kufanya biashara, hatua inayowawezesha kuendesha maisha yao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitaja kwa jina la
Hussein, aliyekuwa akifanya biashara kituo cha daladala cha Mwenge kabla
hakijahamishwa, alisema kabla ya kuondoka eneo hilo, kila siku yeye na wenzake
walilazimika kutoa fedha kwa mgambo ili kupata ridhaa ya kufanya biashara
katika eneo hilo.
“Unajua pale hakukuwepo na utaratibu maalumu wa biashara
hasa kwa sisi tuliokuwa tumeweka meza zetu pembezoni hivyo tulilazimika kulipa
hela kila siku, malipo yalitegemea unaweza ukatoa Shilingi 3,000 hadi Shilingi
7,000 kwa siku hiyo ni kwa kila mtu,” alisema Hussein.
Pia mfanyabiashara mwingine wa Ubungo Darajani, ambaye hata
hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema eneo la Manzese anapofanya
shughuli zake mchana kabla ya kuhamia darajani jioni, analazimika kutoa hela
aweze kufanya shughuli zake.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera,
alipotafutwa kuzungumzia hilo hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi
kutopokewa. Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
akiahidi kulishughulikia suala hilo.
“Tutalifanyia
kazi suala hili kwa kawaida mnapokuwa wengi katika jambo moja wapo
watakaozunguka na kuwakwamisha, hii hali kwa vyovyote ndiyo inayokwamisha
mpango wetu wa kuliboresha jiji hili” alisema Sadiki.
No comments:
Post a Comment