KIKWETE AFANYA ZIARA YA GHAFLA UWANJA WA NDEGE DARRais Jakaya Kikwete, amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo kunakofanyika maandalizi ya kukinga nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha homa hatari ya ebola, ikiwemo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo jana, Rais Kikwete alisema   ameshitukiza makusudi na aliipanga juzi usiku na kuianza jana asubuhi, ili ajionee mwenyewe hatua zilizochukuliwa dhidi ya ugonjwa huo.
"Nimeamua kuja mwenyewe kuona, msikute mnanilisha maneno tu ya uongo kuhusu hatua zinazochukuliwa katika hadhari dhidi ya ebola, sasa nimeona na ninachoomba tumieni pia fursa hii kuboresha," alisema Rais Kikwete ambaye ziara yake ilianzia JNIA na kufuatiwa na Kituo Maalumu Tengefu katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
Mara tu baada ya kutua JNIA, Dar es Salaam, akitokea Dodoma, Rais  Kikwete alikwenda moja kwa moja kukagua vifaa, huduma na maandalizi ya jinsi Tanzania inavyojiandaa kubaini na kushughulikia wagonjwa wa ebola, ambao wanaweza kupitia kwenye uwanja huo.
Rais Kikwete alioneshwa kamera na mashine za kuchanganua picha (Scanners), ambazo tayari zimefungwa kwenye eneo ambalo abiria hulitumia kuingilia katika uwanja huo.Baada ya ukaguzi huo, alitoa  angalizo kwamba hadhari hiyo dhidi ya ebola ifanyike kwa makini, ili isilete shida ya utaratibu kwa wageni na wenyeji wanaoingia au kutoka ndani ya nchi, hususan kupitia viwanja vya ndege.
“Ugonjwa huo usiwe kikwazo kwa abiria kupita kwenye uwanja wetu huu. Tutengeneze mfumo na utaratibu unaowezesha wasafiri kupita katika eneo hilo kama ambavyo imekuwa siku zote, lakini wakati huo huo mashine zetu zikiwa tayari kugundua haraka ni msafiri yupi ana matatizo ama dalili za ugonjwa huo.
“Tusitengeneze mfumo unaozalisha msongamano ndani ya uwanja wa ndege. Napenda kuona wasafiri wanaendelea kuutumia uwanja wetu, bila msongamano na ucheleweshwaji wowote. Abiria wasipate taabu kwa sababu ya ebola,” alisema Rais Kikwete.
Baada ya kumaliza ukaguzi wake katika Uwanja wa Ndege, Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja katika Kituo Kikuu cha Kutenga na Kuhudumia Wagonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Dar es Salaam, katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
“Nimeanzia Uwanja wa Ndege. Nia yangu ni kuona utayari wetu katika kukabiliana na ugonjwa hatari wa ebola, kuona jinsi gani mifumo yetu inavyofanya kazi, kwa ujumla wake, kukabiliana na janga hili hatari sana,” alisema Rais Kikwete ambaye alifuatana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik.
Baada ya kushuhudia maandalizi ya kituo hicho, Rais Kikwete alisema hakina hadhi nzuri na kinahitaji ukarabati zaidi kwani awali majengo hayo yalitengwa kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu.
"Pamoja na hatua mlizochukua za kutenga kituo hiki kuwa cha wagonjwa wa ebola, lakini bado kina upungufu, kwa sababu kilikuwa cha wagonjwa wa kipindupindu na pia kiko karibu na makazi, kingetakiwa kiwe mbali, ila paboresheni pawe pa kisasa kwa hadhi ya nyakati za leo.
“Nataka kuona kituo chenye viwango vya kuhudumia watu wa tamaduni zote na watu wa hadhi zote, kuanzia aliyevaa lubega hadi kwa yule mwenye suti ya sehemu tatu…tena wekeni sehemu ya kupika chakula kwa ajili ya wagonjwa,” alisema Rais Kikwete.
Akijibu hoja hiyo ya Rais, Mratibu wa Huduma za Dharura Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Christopher Mnzava, alisema wameshaomba fedha Hazina Sh milioni 500, fedha ambazo wanazingoja ili kukamilisha ukarabati unaohitajika.
Katika kituo hicho, Rais Kikwete alielezwa kuwa kila mgonjwa mmoja wa ebola ataweza kuhudumiwa na wafanyakazi wanne wa sekta ya afya, ambapo nguo na magauni yao yatachomwa moto kila watakapomaliza kumhudumia mgonjwa.
Pia alielezwa kuwa tayari wanataaluma 1,200 wamepewa mafunzo ya kuhudumia mgonjwa wa ebola katika Mkoa wa Dar es Salaam na vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 119 vimenunuliwa.
Mbali na maandalizi hayo, daktari mmoja ametumwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupata uzoefu wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri Rashid naye alimwambia Rais Kikwete kuwa kitaifa maandalizi yanaendelea na mpaka jana,  ‘Scanners’ tayari zilikuwa zimeshafungwa katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro na Mwanza na katika  vituo vya mipaka ya Tanzania na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia.
Alisema pia maagizo yametolewa kwa hospitali zote nchini kuwa na vyumba maalumu vya kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa wa ebola.
Wiki iliyopita, akizungumza na viongozi na wazee wa Mkoa wa Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mipango,   Rais Kikwete ambaye alikuwa amemaliza ziara ya mkoa huo, alizungumzia tishio la ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana nalo.

No comments: