KESI YA TRAFIKI FEKI YAENDELEA KUPIGWA KALENDAKesi ya aliyejifanya askari polisi wa usalama barabarani, James Hassan (45) imeendelea kupigwa kalenda kutokana na mshitakiwa kutofika mahakamani hapo licha ya kuwepo kwa mashahidi wawili.
Kesi hiyo iliyofikia hatua ya kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imekuwa ikipigwa kalenda mara kwa mara kutokana na mshitakiwa huyo kudai kwamba anaumwa hivyo kukwamisha kesi hiyo kuendelea.
Wakili wa Serikali, Felista Mosha alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma kwamba mashahidi wawili wamefika mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi wao lakini kutokana na mshitakiwa kuwa mgonjwa, aliomba tarehe nyingine ya kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Juma alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 24, mwaka huu kwa hatua za usikilizwaji.
Shahidi wa pili katika kesi hiyo aliieleza Mahakama jinsi mshitakiwa alivyojipatia sare za askari polisi kutoka kwa marehemu baba yake mdogo na kujifanya askari wa usalama barabarani.
Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani Agosti 14, mwaka jana, kujibu mashitaka ya kujifanya askari polisi baada ya kukutwa Kinyerezi Mnara wa Voda na kukana mashitaka hayo. Yupo rumande.

No comments: