JELA MIAKA 15 KWA KUMCHEZEA MTOTO SEHEMU ZA SIRIMahakama ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu kifungo cha miaka 15 jela, Hassan Suleiman (23) mkazi wa Kitunda, kwa kupatikana na hatia ya kumdhalilisha mtoto wa miaka mitatu kwa kumchezea sehemu zake za siri kwa vidole.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassani Juma alisema kuwa mshitakiwa huyo atatumikia kifungo hicho iwe fundisho kwa wengine.
Pia Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kutumia mashahidi wanne ikiwamo mtoto aliyefanyiwa vitendo hivyo pamoja na ushahidi wa fomu ya Polisi ya Matibabu (PF3) iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista Mosha alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 23, mwaka jana, maeneo ya Kitunda Migombani wilayani Ilala ambapo alimwingizia vidole sehemu za siri mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya awali ya Kitunda Mwanagati,  wilayani humo.
Katika utetezi wa awali alioutoa mshitakiwa, alidai mtoto huyo alipotea baada ya kutoka shuleni na kwenda nyumbani kwake kuomba maji ya kunywa ndipo alimueleza Suleiman kwamba amsaidie kumpeleka nyumbani kwao ambako hata yeye mwenyewe hakujui.

No comments: