Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, imezindua kampeni ya kupambana na
saratani ya matiti iliyopewa jina la 'Fanya Sasa, Usisubiri mpaka Oktoba' yenye
lengo la kukuza ufahamu juu ya umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi mapema.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Aidan
Njau alisema kuwa kampeni hiyo imelenga kupiga vita ugonjwa huo ambao umekuwa
ni tatizo kubwa nchini.
Alisema kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi, hospitali hiyo itakuwa ikifanya
kliniki ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti na kutoa elimu lengo likiwa
ni kuwahamasisha watu wapime afya zao haraka badala ya kusubiri mpaka mwezi
Oktoba ambao unajulikana kama mwezi wa saratani ya matiti.
Alisema ili hatua hiyo ilete tija, lazima uchunguzi ugundue saratani kabla
ya dalili kujionesha ambazo humlazimu mtu kutafuta huduma hospitalini.
Alizitaja sababu zinazoweza kusababisha hatari ya kupata saratani kuwa
ni historia ya nyuma juu ya familia, mifumo
ya maisha ikiwemo uvutaji wa sigara, aina za vyakula na historia ya maambukizi
ya virusi na saratani mtu aliyokuwa nayo kwa kipindi cha nyuma.
No comments:
Post a Comment