BOT ILIHUSIKA KUMPATA MZABUNI KUKAGUA DHAHABU, ADAI YONAAliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (73) ameieleza Mahakama kuwa, Benki Kuu (BoT)  ilihusika kusimamia mchakato wa kutafuta kampuni ya kukagua uzalishaji wa dhahabu nchini kwa njia ya zabuni.
Yona alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akijitetea dhidi ya tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Akiongozwa na Wakili wake, Elias Msuya, Yona alidai, waliamua kutafuta kampuni ya kukagua uzalishaji wa dhahabu kutokana na malalamiko ya wananchi na taasisi mbalimbali wakidai kuna tatizo katika Sekta ya Madini.
Alidai wizara yake pamoja na BoT ambayo ilikuwa inasimamia akaunti za kampuni za nje zinazochimba madini nchini, walikubaliana watafute mkaguzi wa uzalishaji wa dhahabu, afanye kazi ya kufuatilia madini yanayochimbwa, gharama na kiasi gani yanauzwa nje ya nchi.
Aliongeza kuwa waliamua BoT ndiyo isimamie mchakato wa kumpata Mkaguzi huyo kwa njia ya zabuni kwa kuwa ndiyo inahusika na utaratibu wa malipo na inasimamia akaunti za makampuni hayo.
Alidai Machi 3, 2003 alimwandikia Rais barua kumweleza kuhusu mapendekezo yao ya kumpata Mkaguzi wa Madini,  Machi 20, Rais alikubali ombi lao na kuwataka waendelee na mchakato huo haraka.
Alidai baada ya kupata kibali cha Rais waliendelea na mchakato huo wakishirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG).
 Mei 20, 2003, alimwandikia tena Rais barua kumueleza  majadiliano kati ya wizara yake, Wizara ya Fedha na BoT yanaendelea vizuri.
Yona alidai, Gavana wa BoT aliandaa Kamati ya kupata Mkaguzi huyo, wizara yake ikiwakilishwa na Godwine Nyelo na wawakilishi wengine kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya AG.
Alidai Novemba 27, 2003, Nyelo alimpa taarifa kuwa wameshampata Mkaguzi huyo lakini hajui walitumia njia gani kumfikishia taarifa mzabuni. Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo Yona atakapoendelea kujitetea.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja.
Wanadaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. 
Ilidaiwa walisababisha hasara hiyo baada ya kutoa msamaha wa kodi kinyume cha sheria kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

No comments: